Habari Mseto

Raia wa Congo kusalia rumande katika kesi ya utapeli wa Sh156m kwenye dili ya madini

April 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Congo anayeshtakiwa kuitapeli kampuni ya kutengeneza chuma Sh156 milioni akidanganya angeliiuzia madini adimu aina ya Tantalum yanayotumika kutengeneza vitonoradi ataendelea kukaa ndani hadi ripoti kuhusu uraia wake iwasilishwe mahakamani.

Afisi ya urekebishaji tabia iliomba muda hadi Aprili 18, 2024 kuwasiliana na nchi za Uganda na Congo kwa vile mshtakiwa yuko na pasipoti mbili na vitambulisho viwili.

“Ripoti ya mshtakiwa haiko tayari. Naomba mudai hadi Aprili 18, 2024 kupokea ripoti kumhusu Lumumba Ulundu Patrick almaarufu Gabriel Kulonda Ulungu almaarufu Lumumba Patrick Byarufu kutoka Uganda na Congo,” hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Bernard Ochoi alifahamishwa na afisa wa idara ya urekebishaji tabia.

Mawakili wanaomtetea mshtakiwa walipinga ombi hilo wakisema “watasaidia kupokea ripoti kutoka kwa nchi hizo mbili.”

Hakimu alimruhusu afisa huyo wa urekebishaji tabia awasiliane na asasi husika kufikia Aprili 16, 2024 atakapotaja tena kesi hiyo.

Lumumba amekana mashtaka mawili ya kula njama za kulaghai kampuni na utapeli wa Dola za Marekani (USD)1,000,000 (KSh156 milioni).

Lumumba aliyekabilliwa na mashtaka hayo mawili aliagizwa azuiliwe katika gereza la Viwandani hadi Aprili 16, 2024 ndipo mahakama iamue ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la.

Lumumba aliomba aachiliwe kwa dhamana lakini kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka alipinga kuachiliwa kwake na dhamana akisema “atatoroka kabisa kwa vile yuko na pasipoti mbili na vitambulisho viwili.”

Mahakama ilielezwa kwamba mshtakiwa aliingia humu nchini akipitia Uganda.

“Mshtakiwa huyu hakutumia pasipoti zake kuingia nchini Kenya. Alitumia pasi maalum inayotumika na mmoja kuzuru mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” Gachoka alimweleza hakimu.

Mahakama ilielezwa ikithubutu kumwachilia mshtakiwa “atatoroka akitumia mojawapo ya pasipoti zilizo na majina tofauti na yale yako kwa kitambulisho.”

Mahakama iliombwa ikatalie mbali ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana kwa sababu “atatoroka bila kujulikana alikoenda.”

Lakini wakili wake alipinga ombi hilo la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kupitia Bw Gachoka akisema “Lumumba ni mkazi wa Mombasa. Polisi wanajua kwake.”

Hakimu alifahamishwa kwa muda wa miaka miwili mshtakiwa amekuwa akiishi humu nchini na “sio kweli hana makazi nchini.”

Akitoa uamuzi hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bernard Ochoi aliamuru mshtakiwa azuiliwe gerezani hadi Aprili 16,2024, atakapoamua kuhusu ombi hilo la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.