Habari Mseto

Raia wa Kenya na Amerika ajitetea kuteuliwa balozi Korea Kusini

May 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MWANADIPLOMAISA Bi Mwende Mwinzi Jumanne alikabiliwa na wakati mgumu kuwashawishi wabunge kwamba anahitimu kuhudumu kama balozi wa Kenya nchini Korea Kusini baada ya kuteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni baada ya kubainika kuwa ana uraia wa Amerika na Kenya. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni ilikuwa ikimpiga msasa mtu ambaye ana uraia wa mataifa mawili.

“Inaonekana kamati hii ndio ya kipekee kuwahi kuchunguza ufaafu mteule wa wadhifa wa umma ambaye alizaliwa katika taifa la kigeni japo mzizi waka uko humo nchini,” akasema Mwenyekiti wa Kamati hiyo Katoo Ole Metito.

Bi Mwinzi ambaye aliwania kiti cha ubunge cha Mwingi Magharibi katika uchaguzi mkuu wa 2017 aliiambia kamati hiyo kwamba japo alizaliwa Amerika, anachukulia Kenya kama nyumbani.

“Japo nilizaliwa Amerika, kwetu ni Kenya. Anaweza kuchagua mahala utaita nyumbani lakini hauwezi kuchagua mahala utazaliwa. Huo ulikuwa uamuzi wa wazazi wangu,” akasema.

Hiyo ndio maana Mbunge wa Mosop akamuuliza hivi: “Sasa ukiidhinishwa kwa wadhifa huu wa balozi wa Kenya nchini Korea Kusini, je, unahudumia Kenya ama Amerika?

Bi Mwinzi akajibu: “Bila shaka nitahudumia Kenya kwa sababu hapa ndipo kwetu. Hii ndio maana niliwania ubunge wa Mwingi Magharibu na kama ningaliibuka mshindi ningewakilisha watu wa eneo hili,”

.Hata hivyo, wabunge wanachama wa kamati hiyo walitaka kujua ni kwa nini Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimwidhinishwa Bi Mwinzi kushiriki uchaguzi mkuu ilhali kufikia Agosti 8, 2017 tarehe ya uchaguzi Bi Mwinzi hakuwa na kitambulisho cha kitaifa cha Kenya.

Stakabadhi alizawalisha mbele ya Kamati hiyo zilionyeha kuwa alipata kitambulisha cha Kenya mnamo Novemba 14, 2017.

Bw Mwinzi, hata hivyo, aliiambia Kamati hiyo kwamba alilazimika kubadilisha kitambulisho chake cha kitaifa kwani “kile ambacho nilitumia katika uchaguzi mkuu hakikuwa na maelezo kamili kunihusu.”

Wengine waliopigwa msasa na kamati hiyo walikuwa Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Michael Mubeo ambaye amependekezwa kuhudumu kama balozi wa Kenya nchini Ireland, Kariuki Mugwe (Abu Dhabi, Muungano wa Milki ya Kiarabu), Peter Katana Angore (Algeria), Flora Karugu (Zambia), Bi Diana Kiambuthi (Scotland) na Bi Njambi Kinyungu (UN Habitat).