Habari Mseto

Raia wa Tanzania ajikuta kwenye kesi ya ulawiti wa mwanabloga Mombasa

Na BRIAN OCHARO October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

IMEBAINIKA kuwa mmoja wa washukiwa waliodaiwa kuhusika katika utekaji nyara na ulawiti wa mwanablogu wa Mombasa ambaye alimkosoa Gavana Abdulswamad Nassir, ni raia wa Tanzania.

Upande wa mashtaka umewasilisha kortini stakabadhi zinazoonyesha kuwa, Bw Abdul Hassan Athman almaarufu kama Sindimba ni raia wa kigeni.

Upande wa mashtaka sasa unataka mahakama izingatie hilo itakapoamua ombi la dhamana za washtakiwa hao wanne.

“Ni kweli imethibitishwa kwamba Athman ni raia wa Tanzania. Tunaitaka mahakama kuzingatia ukweli huu wakati wa kubainisha iwapo ni salama kumwachilia kwa dhamana,” Kiongozi wa mashtaka, Bw Anthony Musyoka aliambia mahakama ya Shanzu.

Bw Athman alishtakiwa pamoja na Haji Babu Ndau Mohamed almaarufu kama Achkobe au Jay, Bi Esther Muthoni John almaarufu kama Totoo na Bi Violet Adera almaarufu kama Vayoo kwa makosa ya utekaji nyara na ulawiti uliotekelezwa na watu wengi.

Vilevile, walikabiliwa na shtaka la kupanga njama ya kutenda kosa ambapo serikali ilidai kuwa, washukiwa hao wanne walipanga njama ya kumteka nyara mwanablogu aliyetambuliwa mahakamani kama BJK kwa nia ya kumweka kizuizini.

Mahakama ilisikia kuwa, washukiwa hao walimteka nyara mwathiriwa katika eneo la Bamburi Jitegemee huko Kisauni.

Mabw Athman na Mohamed wanashtakiwa tofauti kwa kosa la ulawiti uliotekelezwa na watu wengi, ambapo wanatuhumiwa kumnyanyasa kingono BJK na pia kumshambulia mwathiriwa.

Mahakama ilisikia kwamba mnamo Septemba 12, mwaka huu, washukiwa hao waliingia ndani ya nyumba ya mwathiriwa na kumshawishi aende nao katika hoteli ya mjini, ambako alitarajiwa kumuomba radhi gavana kwa video hizo za kukera.

Kabla ya tarehe hii, BJK alikuwa amerekodi video na kuchapisha kwenye mtandao wa TikTok, akimkosoa gavana Nassir.

Mahakama ilielezwa kuwa, siku ya kutekwa nyara, genge hilo lilimfahamisha BJK kuwa maudhui ya video yake yalikuwa yanaharibu sifa ya Nassir lakini alihitajika tu kuomba msamaha.

“Alitekwa nyara akiwa anaelekea katika hoteli hiyo.Kulikuwa na pikipiki nyingine sita, kila moja ikiwa na abiria,” Koplo Irene Karuga, anayechunguza kisa hicho aliiambia mahakama.

Jamaa huyo alilazimishwa kuingia kwenye gari aina ya Toyota Vitz lililokuwa likimsubiri na kukimbizwa hadi mahali ambapo alidhulumiwa kabla ya kufunikwa kwenye gunia.

Uhalifu huu iliendelea kwa dakika kadhaa huku BJK akiomba genge hilo kumhurumia. Hata hivyo, genge hilo liliendelea na uhalifu huo likimzomea anyamaze.

Wakati BJK akihema kwa maumivu, genge hilo lilishangilia kitendo hicho huku wakimcheka. Baadhi ya genge hilo pia lilikuwa likirekodi video za kitendo hicho kiovu.

“BJK aliendeshwa huku na huko, na alipofika eneo la Mwakirunge, alitupwa akiwa amepoteza fahamu,” alisema Bi Karuga.

BJK aliwaambia polisi kwamba, baada ya genge hilo kumaliza kumnyanyasa kingono, alisikia mazungumzo ya simu yakimjulisha mtu kwamba walikuwa wamemaliza kazi hiyo.

“Genge hilo lilielekezwa kukaa na mlalamishi mchana na usiku mzima. Pia walipaswa kupokea kiasi fulani cha fedha kusheherekea mlo wa jioni na matumizi mengine ya anasa wakati wa operesheni hiyo,” afisa huyo alisema katika hati zake za mahakama.

Mhudumu wa bodaboda aliyembeba BJK kutoka eneo alilotupwa alilipwa na msamaria mwema ambaye pia alimshauri atafute matibabu.