Raila awatema washauri wenye misimamo mikali ili kujisuka upya kisiasa
Na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa chama cha ODM Bw Raila Odinga Jumatano amelazimika kuwatema washauri wake waliokuwa na misimamo mikali ili kufanikisha muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta na kujisuka upya kisiasa.
Wadadisi wanasema kwa sasa, Bw Odinga atategemea washauri wachache nje ya familia yake ambao hawana misimamo mikali kama wale aliokuwa akitegemea kabla ya muafaka wake na Rais Kenyatta.
“Raila hakuwa na budi kubadilisha washauri wake, hangekubaliana na Uhuru kama angekuwa na waliokuwa na misimamo mikali hasa wakati wa kampeni za uchaguzi 2017,” akasema mchanganuzi wa siasa Danstan Omari alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali.
Miongoni mwa washauri aliokuwa akiwategemea kabla ya kutangaza muafaka wake na Rais Kenyatta Machi 19 ni seneta wa Siaya James Orengo, wakili Norman Magaya, mwanauchumi Dkt David Ndii na maafisa wa chama chake cha ODM na muungano wa NASA.
Aidha, wakati wa kujiapisha kwake kama rais wa wananchi Januari 30, 2018, alikuwa akitegemea ushauri wa wanasiasa wa chama cha ODM kama vile seneta Orengo, wabunge T J Kajwang, Antony Olouch, Edwin Sifuna na hata wakili Dkt Miguna Miguna.
Walipokuwa wakitangaza muafaka wao kwa nchi nje ya ofisi ya rais, Bw Odinga aliandamana na mbunge wa Suna Mashariki Bw Junet Mohamed na binti yake Winnie Odinga.
Akihojiwa na mwanahabari Joe Ageyo mwishoni mwa mwaka jana nyumbani kwake Bondo, Bw Odinga alisema mazungumzo yake na Rais Kenyatta yalifanikiwa kwa sababu ya kutohusisha watu wengi. “Kama kuna watu waliohusika kabla ya kukutana na Rais Kenyatta, hawawezi kuzidi wawili, mmoja kutoka kila upande” alisema Bw Odinga bila kufafanua.
Baada ya kutangazia nchi muafaka wao, Bw Odinga alibadilisha mkondo wake wa kisiasa kabisa na kujitenga na waliokuwa washirika wake wa karibu wa kisiasa.
Wadadisi wanasema amekuwa karibu sana na familia yake huku kaka yake Dkt Oburu Odinga, mkewe Ida na binti yake Winnie wakitekeleza jukumu kubwa katika maamuzi yake ya kisiasa.
Nje ya familia, Bw Odinga amekuwa akimpa sikio Bw Junet, wakili wake Paul Mwangi, Gavana wa Kisumu Profesa Peter Anyang Nyongo na mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga.
Kwa kuwatema washauri wake wa kisiasa waliokuwa na misimamo mikali, Bw Odinga amefaulu kuweka mwelekeo wake wa kisiasa kuwa siri sawa na mazungumzo yaliyopelekea muafaka wake na Rais Kenyatta.
Kiongozi huyo wa upinzani amepunguza vikao vyake na wanahabari tangu aingie kwa muafaka na Rais Kenyatta.