Rais hafai kukosolewa akiteua mawaziri – Mahakama
Na RICHARD MUNGUTI
KATIKA uamuzi wa kihistoria, Mahakama ya Kuamua Mizozo ya Wafanyakazi (ELRC) imesema Rais Uhuru Kenyatta hapasi kukosolewa au kuhojiwa mahakamani kwa uteuzi wa mawaziri na watumishi wengine wakuu serikalini.
Mahakama ilisema katiba imewapa wananchi mamlaka ya kumchagua wanayempenda kuwa akitekeleza majukumu fulani kwa niaba yao.
Jaji Nelson Abuodha alisema Rais Kenyatta hutekeleza majukumu yake miongoni mwao kuwateua watumishi wa umma “ kutokana na mamlaka aliyopewa na wananchi waliomchagua.”
Jaji Abuodha alisema katiba inasema nguvu na mamlaka ni ya wananchi na inaweza kutekelezwa na yule aliyechaguliwa na wananchi kama vile Rais Kenyatta.
Hata hivyo Jaji Abuodha alitahadharisha uteuzi wowote unaofanywa na Rais haupasi kuwa wa kuwatunuku au kuwalipa wale walio na maoni sawa ya kisiasa ama wale waliotekeleza jukumu fulani ya kisiasa.
Jaji Abuodha aliyekataa kuwatimua kazi maafisa wawili wakuu katika idara ya Magereza ambao waliteuliwa na Rais Kenyatta kuhudumu kwa muda wa miaka miwili zaidi baada ya kuhitimu umri wa wa kustaafu wa miaka 60, alisema sheria za kuajiri watumishi wa umma zinamruhusu kuongezea muda walio na ujuzi maalum.
Jaji Abuodha aliamuru Mabw Isaya Osugo na Omar Tawane Gudai waendelee kuhudumu hadi kipindi chao kikamilike.
Wawili hawa waliongezewa muda wa kuhudumu mnamo Juni 29, 2016.