Rais Kenyatta awatumia Waislamu risala za heri Ramadhani
DIANA MUTHEU na WINNIE ATIENO
RAIS Uhuru Kenyatta amewahimiza Waislamu waombee nchi watakapokuwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoanza rasmi Alhamisi.
Kwenye ujumbe wake wa heri njema kwa Waislamu Jumatano, alisema Kenya inahitaji maombi ya kila mmoja, na huu ndio wakati mwafaka kwa waislamu kuzidisha maombi.
“Kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Kenya, ninawatakia heri njema na tunaungana na ndugu zetu waumini wa Kiislamu mnapoanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ni nguzo muhimu katika dini ambayo inawafunza umuhimu wa nidhani, upole na kujitolea,” akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Rais Kenyatta aliwahimiza Wakenya wengine kuungana na Waislamu katika kuendeleza mshikamano wa nchi, na kuachana na tofauti ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikiigawa nchi.
Wakati huo huo, polisi mjini Mombasa na eneo zima la Pwani wameahidi kushika doria katika maeneo ya ibada, hasa zitakazoendelezwa nyakati za usiku.
Maafisa wakuu wa usalama eneo la Pwani, wakiongozwa na kamanda wao, Bw Noah Mwivanda, walisema polisi watatumwa katika maeneo ya ibada, hasa misikitini kudumisha amani na utulivu.
Pia, idara ya polisi imeweka hatua madhubuti kuzuia uhalifu na kuimarisha upelelezi katika maduka makubwa, maeneo ya kujistarehesha, taasisi za elimu, vivutio vya utalii, barabara kuu na vituo vya mabasi katika eneo la Pwani.
“Maeneo hayo yatakuwa na usalama wa kutosha na yatalindwa vilivyo. Tumeweka hatua zote kuhakikisha Ramadhani inaadhimishwa bila utovu wa usalama. Maeneo yote ya ibada yatakuwa na maafisa wa polisi wa kutosha,” alisema.
Aliwahimiza wakazi kuripoti visa vya uhalifu karibu na makazi yao.