Habari Mseto

RIBA: Wabunge wengi wasusia kikao cha asubuhi

November 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

BUNGE Jumatano limeahirisha kikao cha asubuhi mapema baada ya wabunge wengi kukosa kufika ukumbini katika kile wametaja ni kuonyesha ghadhabu yao kutokana na kile walichodai ni mazoea ya Rais Uhuru Kenyatta kuhujumu uhuru wa asasi hiyo.

Spika wa muda Christopher Omulele alisitisha vikao vya mwendo wa tano baada kujulishwa kwamba kulikuwa na wabunge 15 kwenye ukumbi wa mijadala badala ya angalau 50, kulingana na kanuni za bunge.

Ilisemekana kuwa wabunge wamechelea mijadala bunngeni kwa kukasirishwa na hatua ya Rais kurejesha Mswada wa Fedha 2019 kwao akipendekeza kuondolewa kwa kipengee cha kudhibiti viwango vya riba vinavyotozwa na benki kwa mikopo.

Lakini mnamo Jumanne wabunge hao walishindwa kubatilisha pendekezo hilo la Rais kwani kulikuwa na wabunge 161 pekee suala hilo lililopokuwa likishughulikiwa.

Kwa mujibu wa Katiba pingamizi ya Rais kuhusu mswada uliopitishwa bungeni inaweza tu kubatilishwa na thuluthi mbili ya wabunge wote 349, yaani angalau wabunge 233.

Pendekezo la Rais lapita

Kwa hivyo, ukosefu wa idadi tosha ya wabunge siku hiyo ulimaanisha kuwa pendekezo la Rais lilipita na benki sasa ziko huru kutoza riba zinazotaka kwa mikopo zitakazotoa kwa wateja wao baada ya Rais kutia saini mswada huo.

Jana, kiranja wa wengi Benjamin Washiali aliungama kuwa wabunge walikwepa kikao cha asubuhi kwa kukasirishwa na hatua ya rais kuingilia wajibu wao wa utungaji wa sheria.

“Inaonekana kuwa wabunge wamesinywa na hizo memoranda za kila mara kutoka Ikulu kubatilisha vipengee muhimu katika miswada wanayopitisha. Wanataka uhuru wa kuendesha wajibu wao wa kutunga sheria bila kudhibitiwa wala kuingiliwa na mtu au asasi yoyote,” Bw Washiali, ambaye ni mbunge wa Mumias Mashariki, amewaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Mnamo Jumanne, wabunge waliondoka bungeni kwa hasira baada ya Spika Justin Muturi kutangaza kuwa sheria inayoziruhusu benki kutoza viwango vya riba zinavyotaka imepita, hii ikiwa ni baada ya kukosekana kwa idadi tosha ya wabunge kubatilisha pendekezo la Rais kwa mswada wa Fedha 2019.

Katika memoranda aliyoiwasilisha bungeni, Rais Kenyatta alisema aliamua kuondoa sheria ya udhibiti wa riba kwani chini ya sheria hiyo benki nyingi zilikataa kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo.

Kwa upande mwingine, serikali ilikuwa ikikopa kwingi kutoka kwa benki za humu nchini na hivyo kuinyima sekta ya biashara ndogondogo (SMEs) nafasi ya kupanuka.