Rift Valley Railways yawekewa vikwazo na IMF sababu ya ufisadi
Na BERNARDINE MUTANU
BENKI ya Dunia imeliwekea vikwazo Shirika la Uchukuzi wa Reli la Rift Valley Railways (RVR).
Hii ni kutokana na ufisadi mwingi unaolizonga shirika hilo kutokana na mkataba wa ushirikiano kati ya mashirika ya uchukuzi wa reli ya Kenya na Uganda.
Benki ya Dunia ilichukua hatua hiyo baada ya visa vya ufisadi katika miradi inayofadhiliwa na tawi la kibinafsi la Benki ya Dunia-International Finance Corporation (IFC).
RVR iliwekewa vikwazo pamoja na mashirika mawili, ambapo moja ya mashirika hayo lilipigwa marufuku kushiriki katika miradi ya Benki ya Dunia kwa miaka miwili. Shirika hilo ni Africa Railways Logistics Ltd.
Kulingana na benki hiyo, afisa wa shirika hilo alipatikana kushawishi utaratibu wa forodhani kutoa idhini kwa uingizaji wa magari ya moshi ambayo yalikuwa sehemu ya miradi miwili IFC, ilisema katika taarifa.
Kampuni za Africa Railways Ltd na Rift Valley Railways Kenya, (RVRK) pia ziliwekewa vikwazo lakini kwa masharti. Zinaweza kushiriki miradi ya Benki ya Dunia ikiwa zitafuata taratibu, kanuni na masharti ya benki hiyo kulingana na mkataba.
RVRK imekubali kwamba afisa mmoja alivunja taratibu za kandarasi hiyo. Tayari, shirika hilo limemfuta kazi afisa huyo, ambaye alikuwa na kampuni iliyokuwa ikimezea mate mapato kutokana na kandarasi hiyo kwa kuwa na kampuni yake iliyokuwa ikishiriki katika kandarasi hiyo kupitia kwa RVRK.