Habari Mseto

Ripoti ya UNDP yaonyesha idadi ya vifo vinavyosababishwa na uchafuzi mazingira viko juu Kenya

January 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

KENYA inakumbwa na athari mbaya za uchafuzi wa mazingira ambapo watu 165 wanafariki kila siku kutokana na hali hiyo.

Kulingana na ripoti ya shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa – United Nations Development Programme – (UNDP) ambao ni mtandao wa maendeleo duniani, uchafuzi huo wa mazingira umekuwa mbaya zaidi hasa kutokana na uharibifu wa misitu.

Kenya inakadiriwa kupoteza asilimia 5.8 ya misitu kila mwaka.

“Vifo vinavyosababishwa na uchafuzi wa hewa ni watu 78 kwa kila watu 100,000 huku vifo vinavyosababishwa na maji machafu na uchafu katika mazingira ukifikia 51.2 katika idadi hiyo ya watu,”  inasema taarifa hiyo yenye jina ‘Human Development of 2018 revealed’.

Idadi ya watu nchini Kenya ni 47 milioni na hivyo idadi hiyo inatafsiriwa kuwa watu 36,600 wanafariki kutokana na uchafuzi wa mazingira huku wengine 23,970 wakifariki kutokana na hali mbaya ya usafi wa mazingira.

Kenya ni baadhi ya nchi zinazoendelea ambazo zinatoa kiwango cha chini cha hewa kaa – carbon – ikilinganishwa na nchi kama Amerika.

Mkurugenzi wa shirika la Kenya Meteorological Services Bi Stella Aura katika taarifa alisema kuwa uchafuzi huo unachangia katika madhara makubwa katika usalama wa chakula, afya na uhai wa wanyama wa majini.

Aliongeza kuwa baadhi ya athari ni kama vile ongezeko la joto jingi katika baadhi ya maeneo kama vile pwani mwa Kenya.