Habari MsetoSiasa

Rotich aitwa bungeni kueleza kiini cha fedha za CDF kuchelewa

February 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na GEORGE MUNENE

WAZIRI wa Fedha Henry Rotich ametakiwa kufika mbele ya wabunge wiki hii kuelezea sababu za kucheleweshwa kwa pesa za Hazina ya Ustawi wa Maeneo-bunge (CDF), baada ya kubainika kuwa hazina hiyo imepokea Sh6.38 bilioni pekee kati ya Sh33.28 bilioni ilizotengewa mwaka 2019.

Spika wa Bunge Justin Muturi Jumanne aliamuru Kamati ya Bunge kuhusu CDF iandae vikao na Waziri Rotich kisha iwasilishe ripoti yake kwa bunge.

“Haiwezekani kwamba ikisalia miezi minne pekee kabla ya kukamilika kwa mwaka huu wa kifedha, 2018/2019, ni Sh6.38 bilioni pekee ndizo zimeelekezwa kwa hazina ya CDF. Hili ni suala zito na bunge linapaswa kupata ufafanuzi kupitia Waziri wa Fedha,” akasema Bw Muturi.

Alitoa amri hiyo baada ya mwenyekiti wa kamati ya CDF, Bw Maoka Maore kuwasilisha ripoti kuhusu usambazaji wa pesa za hazina hiyo.

Kulingana na mbunge huyo wa Igembe Kaskazini kufikia mwezi Oktoba 30, 2018, Bodi ya Kitaifa ya CDF ilikuwa imepokea Sh10.3 bilioni pekee kutoka kwa Hazina ya Kitaifa. “Sh4 bilioni kati ya fedha hizo ni malimbikizo ya madeni ya kuanzia mwaka wa 2011 huku Sh6.38 bilioni zikiwa sehemu ya mgao wa mwaka huu kutoka kwa bajeti ya kitaifa ambayo ni Sh33.28 bilion,” akasema.

Bw Maore alisema sehemu ya fedha ambazo CDF imepokea kufikia sasa inawakilisha asilimia 19 pekee ya mgao wote kwa hazina hiyo katika mwaka huu wa kifedha wa 2018/2019.

Kiongozi wa Wachache John Mbadi alisema kucheleweshwa huko kwa pesa za CDF kunaashiria kuwa serikali imefilisika akiongeza kuwa changamoto hiyo pia inazikumba serikali za kaunti.

Umeme

Kwingineko, mamia ya polisi wanaohudumu katika Kaunti ya Embu wanakaa gizani baada ya umeme katika nyumba walimokuwa wakikaa kukatwa. Hili ni kufuatia kuisha kwa muda ambao walikuwa wamepewa kuondoka katika nyumba za serikali.

Umeme huo ulikatwa mnamo Jumatatu na maafisa wa Kampuni ya Umeme (KP) wakiwa wameandamana na maafisa wakuu wa polisi wa Kaunti.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kwamba nyumba zote za polisi katika Kituo cha Polisi cha Embu Magharibi hazikuwa na umeme.

Hali hiyo ni sawa katika vituo vingine vya polisi katika eneo hilo, kulingana na polisi mmoja ambaye hakutaka kutajwa.

“Walifika katika laini zilizounganisha stima na kuzikata hata bila kutujulisha,” akasema. Polisi wengine walisema kwamba hatua hiyo ilichukuliwa bila kuwaarifu, huku wakiilaumu KP kwa kutowajibika.

Vilevile walilalama kwamba ni kama wanalazimishwa kuhama nyumba hizo, kwani mmoja wa wakuu wao ni miongoni mwa wale wanaoendesha shughuli hiyo. Walilalama kwamba hali hiyo imezifanya familia zao kuteseka bila sababu zozote.

“Huwa tunatumia stima kupikia, kuchaji simu, kupiga pasi nguo zetu kati ya shughuli nyingine. Hali ni mbaya sana sasa. Hatuikubali kamwe,” akasema polisi mwingine. Polisi hao walisema wako tayari kulipa bili za umeme, ikiwa KP itawapa taarifa za madeni yao.