• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Ruto akutana na Feisal baada ya kushinda kiti cha Msambweni

Ruto akutana na Feisal baada ya kushinda kiti cha Msambweni

 Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto Jumatano alifanya mkutano na viongozi wa mashinani kutoka eneo bunge la Msambweni wakiongozwa na mbunge wao mpya Feisal Bader katika makazi yake rasmi Karen, Nairobi.

Bw Bader Jumanne aliapishwa rasmi kama Mbunge wiki moja baada ya kushinda kiti hicho alipombwaga mgombeaji wa ODM Omar Boga, mnamo Desemba 15. Bader alizoa kura 15,251 huku Boga akipata kura 10,444.

Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori mnamo Mach 9, 2020

Kwenye ujumbe aliyoweka katika kaunti yake ya twitter baada ya kukubana na ujumbe huo kutoka Msambweni, Dkt Ruto alisema kuwa uchaguzi huo mdogo ulifungua sura mpya katika siasa za Kenya.

“Sasa wananchi wamethibitisha kuwa hawawezi kuathiriwa na majina makubwa yanayomuunga mkono mgombeaji fulani. Wananchi wameng’amua kuwa wao ndio wenye uwezo wa kuamua viongozi wao kwa misingi ya utendakazi ambao unaolenga kutimiza matakwa na ndoto za raia,” Dkt Ruto akasema.

Wengine walioandamana na Bw Bader ni Mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani, Nixon Korir (Langata) na aliyekuwa Mbunge wa Starehe Askofu Margaret Wanjiru.

Bw Bader alisema atalenga kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na marehemu Dori ambaye ni mjombake.

Mbunge huyo alitoa shukrani zake kwa Naibu Rais na wandani wake waliomuunga mkono kwa dhati wakati wa kampeni.

“Naibu Rais alisimama name wakati ambapo ODM ilinidhulumu. Washirika wake wa karibu kama vile Muthama (Seneta wa zamani wa Machakos), Boni Khalwale (Seneta wa zamani wa Kakamega) na Hassan Omar alipiga kambi Msambweni kuhakikisha kuwa ninashinda. Ninajua siwezi kuwalipa lakini nitazidi kuwaombea,” akasema.

Dkt Ruto aliamua kumuunga mkono Bader aliyewania kiti hicho bila kudhaminiwa na chama chochote cha kisiasa baada ya chama cha Jubilee kutangaza kuwa hakitadhamini mgombeaji na kwamba kitaunga mkono Bw Boga.

You can share this post!

Trippier kutumikia marufuku ya wiki 10 kwa kukiuka kanuni...

Kamata kamata ya polisi kwa wasiovalia maski Krismasi...