Ruto awataka polisi kutotumia nguvu kupita kiasi wanapotekeleza kafyu
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto amewataka maafisa wa polisi kutotumia nguvu kupita kiasi wanapohakikisha wananchi wanazingatia amri ya kutotoka nje ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Hata hivyo, amesisitiza Jumamosi kuwa kila mwananchi anapaswa kutii agizo la kutoonekana nje kuanzia saa moja usiku.
“Walinda usalama sharti watekeleze wajibu wao, lakini sio kwa ukatili. Na wananchi nao hawana budi kutii agizo lilotangazwa na serikali la kutotoka nje kuanzia saa moja usiku ili kudhibiti janga hili la virusi vya corona,” Dkt Ruto amesema kupitia chapisho lake katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter.
Naibu Rais alikuwa akijibu malalamishi ya viongozi na wananchi kufuatia visa mbalimbali ambapo polisi waliwashambulia raia kikatili katika harakati za kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.
Picha kadhaa zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha polisi wakiwapigwa raia kwa rungu, mijeledi, na vitoa machozi huku wengine wakiwarushia matusi.
Dkt Ruto amesema janga la Covid-19 ni hatari na hivyo masharti yaliyowekwa kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo ni sharti yazingatiwe na kuchukuliwa kwa uzito.
“Wananchi wenzangu, mkurupuko wa virusi vya corona ni hatari; hatari zaidi. Kafyu iliyotangazwa na serikali inalenga kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo,” Dkt Ruto akaeleza.