• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Ruto pia asusia kongamano la madiwani

Ruto pia asusia kongamano la madiwani

Na PETER MBURU

NAIBU Rais William Ruto Jumatano alifuata mkondo wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, kususia kongamano la madiwani, ambalo lilikamilika Jijini Kisumu.

Dkt Ruto alitarajiwa kufunga kongamano hilo rasmi katika hoteli ya Grand Royal Swiss, lakini hakufika.

Hatua yake ya kutohudhuria ilifuata ile ya Rais Kenyatta kulisusia baada ya kutarajiwa kulifungua rasmi Jumatatu, na pia Bw Odinga ambaye alitarajiwa kulihutubia Jumanne. Japo Rais aliwakilishwa na Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa, Dkt Ruto na Bw Odinga hawakuwakilishwa.

Kutojitokeza kwa viongozi hao wakuu, ambao walitarajiwa kwa hamu kabla ya kuanza kwa kongamano hilo, kuliwaacha wengi bila kujua sababu zao za kulisusia.

Kongamano hilo ambalo lilikuwa limeleta pamoja madiwani kutoka kaunti zote nchini, maspika wa mabunge ya kaunti na viongozi katika bunge la seneti, wakiongozwa na Spika Kenneth Lusaka, lilikamilika jana, baada ya kikao cha siku tatu.

Masuala mbalimbali kama changamoto za uongozi ambazo zimekuwa zikikumba mabunge ya kaunti ni baadhi ya mambo ambayo yalijadiliwa kwa kina.

Madiwani walitumia kongamano hilo la nne kushinikiza wapewe fedha za kununua magari. Siku ya kwanza ya kongamano hilo, madiwani walikatiza hotuba ya Seneta Maalumu, Dkt Agnes Zani wakitaka ahadi waliyopewa mnamo 2013 ya kupewa fedha za kununua magari itekelezwe.

Madiwani wanapinga kupewa fedha za mkopo za kununua magari.

Madiwani hao pia walilalamikia kucheleweshwa kwa mswada utakaohakikisha kuwa wanatengewa fedha za ustawishaji wadi.

You can share this post!

Moraa ashindia Kenya dhahabu ya tatu Riadha za Afrika

Aliyemtishia ripota wa NMG azuiliwa na polisi

adminleo