Habari Mseto

Sababu za wafanyabiashara kuandamana Jogoo Road

Na SAMMY KIMATU March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HALI ya utulivu imerejea baada ya zaidi ya wafanyabiashara 300 wa Juakali katika soko la Uhuru, Jogoo Road, jijini Nairobi kushiriki maandamano mnamo Jumanne, Machi 18, 2025.

Waandamanaji waliwasha magurudumu barabarani na kutatiza shughuli za usafiri.

Msongamano mkubwa wa magari ulishuhudiwa kabla ya maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia na wenzao waliovalia kiraia kutoka kituo cha Polisi cha Jogoo, Makongeni na cha BuruBuru kutawanya waandamanaji kwa kuwafyatulia vitoza machozi.

Naibu Kamishna wa kaunti Ndogo ya Makadara Bw Philip Koima aliongoza maafisa wengine wa Kaunti katika kamati ya usalama kuhutubia wafanyabiashara hao waliojawa na gadhabu.

Ilibainika kuwa wafanyabiashara wa soko la Juakali walipinga notisi ya kuhamishwa kutoka kwa soko hilo na serikali ya kaunti ya Nairobi.

Vilevile, Bw Koima aliongeza kwamba wafanyabiashara hao walidai hawakushirikishwa kwa mkutano sawia na hawakupewa muda wa kutosha kuondoka.

Hayo yakijiri, Bw Koima alisema baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakieneza propaganda kwamba ardhi ya soko ilikuwa imeuzwa kwa mwekezaji wa kibinafsi.

“Madai haya yalithibitishwa kuwa hayaeleweki na yaliwasilishwa kwa wafanyabiashara walioathirika ipasavyo,” akasema afisa huyo.

Kulingana na Bw Koima, wafanyabiashara wengine pia walidai kupewa nafasi mbadala ya kuuza bidhaa zao.

Hata hivyo walionywa na Bw Koima kuachana na vitendo vya uhalifu, hasa uharibifu wa barabara na miundomsingi mingine muhimu kwa kisingizio cha kufanya maandamano. Kadhalika, walishauriwa kufuata utaratibu wa kisheria na kukumbatia amani kutatua migogoro.

Bw Koima alitoa onyo kali dhidi ya magenge ya uhalifu waliokuwa wakivizia wananchi kufanya uhalifu na vitendo vingine viovu vya uvunjaji sheria.