Sabina Chege apinga mpango wa elimu mashinani
Na MWANGI MUIRURI
MWENYEKITI wa kamati ya bunge la kitaifa kuhusu afya Bi Sabina Chege ameshabikia hatua ya mahakama kuu kutoa ilani ya kusimamisha mpango wa elimu mashinani uliokuwa uzinduliwe kesho Ijumaa.
Jaji James Makau mnamo Jumanne aliagiza mpango huo ambao unajumuisha walimu katika eneo moja mashinani kusajiliwa na kisha hata chini ya miti watoto wawe wakijumuika kuelimishwa.
Kupitia ombi la mzazi Joseph Aura kuwa mpango huo haufai kamwe na shule zinafaa kufunguliwa ili kuwapa watoto wote nafasi sawa ya kuafikia elimu, Jaji Makau aliorodhesha kesi hiyo kuwa ya dharura na akaamua mpango huo wa Waziri George Magoha kwanza usimamishwe hadi kesi iskizwe na kuamuliwa.
Kwa upande wake, Bi Chege akiongea katika hospitali kuu ya Murang’a amesema waziri Magoha hana ule uwezo wa kujadiliana na huwa anatekeleza masuala yake kimabavu.
Aidha, amesema kuwa Bw Magoha huwa hana ule uvutio kwa ushirikishi, akisema kuwa “mpango huu wa elimu mashinani haukuzingatia malalamiko mengi ya wadau.”
Katika hali hiyo, Bi Chege ameshabikia amri hiyo ya mahakama akiomba Magoha sasa aandae vikao vya wadau ili kupiga msasa mpango huo.
Magoha amekuwa akisisitiza kuwa watoto wakibakia wa kurandaranda mitaani bila ya juhudi zozote za kuwaweka na majukumu na elimu ni sawa na kuwatuma katika jangwa la kila aina ya utukutu na ambao utaishia kuwapa kila aina ya hatari kama mimba za mapema, utumizi wa mihadarati na kuingia katika magenge haramu.
Bi Chege alisema kuwa hapingani na wazo hilo bora la waziri Magoha “lakini wazo lizuri likitekelezwa bila utiifu kwa ushirikishi na bila kuzingatia hatari zilizoko ni sawa tena na kuwatuma ndani zaidi ya jangwa hilo hatari.”
Alisema kuwa ugonjwa wa Covid-19 umesambaa mashinani hivyo “ni lazima tuhakikishe kuwa utangamano wa watoto wetu hautazua hatari zaidi ikizingatiwa kuwa wengi wa walioambukizwa hawaonyeshi dalili zozote lakini wanaweza wakaambukiza wengine.”
Amependekeza waziri Magoha aandae kikao cha wadau na kupiga msasa hatari hizo na kisha uamuzi wa mwisho uwe ni ule unaozingatia hata ushauri wa kitaalamu kutoka Wizara ya Afya.
“Mimi ni mwalimu kitaaluma na sielewi ni jinsi gani walimu watakuwa wakielimisha watoto wa gredi tofauti kwa wakati mmoja,” amesema Bi Chege.
Akahoji: “Ikiwa wanafunzi wa gredi ya tatu watajitokeza wakiandamana na wengine wa darasa la nane au la sita, watawekwa chini ya mfumo gani wa kielimu? Ama Magoha anapendekeza wanafunzi hao wakijumuika pamoja wawe wakicheza, kuimba au kufunzwa jinsi ya kukaa pamoja?”