Habari MsetoSiasa

Saburi kulala ndani hadi Alhamisi

April 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na PHILIP MUYANGA

NAIBU Gavana wa Kilifi Gideon Saburi, ataendelea kukaa kizuizini katika kituo cha polisi cha Port jijini Mombasa hadi Alhamisi.

Hii ni baada ya Mahakama ya Mombasa kusema siku hiyo ndiyo itatoa uamuzi wake wa iwapo itakubali ombi la upande wa mashtaka kuwa Bw Saburi azuiliwe katika Gereza la Manyani kwa siku 14.

Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP) ilikuwa imeomba Bw Saburi azuiliwe peke yake katika gereza hilo lililoko Voi, Kaunti ya Taita Taveta ili kuwawezesha maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi.

Kupitia kwa waonmgoza mashtaka Edgar Mulamula na Anthony Musyoka, DPP ilisema kuwa uchunguzi bado haujakamilika kwa kuwa mashahidi kutoka maeneo ambayo naibu gavana huyo alizuru bado hawajaandika taarifa zao.

Bw Mulamula alimwambia Hakimu Mkuu Mkazi wa Mombasa Ritah Amwayi kuwa Bw Saburi alikuwa ametia sahihi stakabadhi katika uwanja wa ndege kuwa atajitenga alipowasili nchini, lakini bado hawajapata stakabadhi hiyo.

“Kuna watu wanaugua Covid-19 katika Kaunti ya Kilifi na tumepata habari kuwa wakazi wamekasirishwa na vitendo vya Naibu Gavana, hivyo wangetaka kumdhuru. Ndiposa tunataka akae kizuizini,” alisema Bw Mulamula.

Kupitia mawakili wake George Kithi na Clifford Tollo, Bw Saburi alipinga ombi hilo akisema halikuwa limewasilishwa mahakamani inavyohitajika.

“Hatua ya kujaribu kumzuia mtu gerezani kabla ya kujibu mashtaka haijawahi kusikika,” akasema Bw Kithi.

Aliongeza kuwa naibu gavana huyo hajawahi kupatikana na ugonjwa wa Covid-19 na kwamba hakuna stakabadhi yeyote ya hospitali inathibitsha jambo hilo.

“Hajawahi kupatikana na Covid-19, na hajaambukiza mtu yeyote,” alisema Bw Kithi akiongeza kuwa uchunguzi uliofanyiwa Bw Saburi mara tatu ulionyesha hakuwa na Covid-19.

Wakili huyo alipuuza madai ya upande wa mashtaka kuwa Bw Saburi atapigwa na raia iwapo ataachiliwa kutoka kizuizini, akisema kuwa hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa maisha ya Bw Saburi yako hatarini.