SAKATA YA HONGO BUNGENI: Wabunge 15 kuchunguzwa
Na CHARLES WASONGA
BAADA ya kuahirishwa mara kadha, hatimaye uchunguzi kuhusu madai ya aibu ya wabunge kupokea hongo ya kati ya Sh10,000 na Sh30,000 ili kuangusha ripoti kuhusu sakata ya sukari utaanza bungeni Jumanne ambapo wabunge 15 wameratibiwa kuhojiwa.
Kamati ya Mamlaka na Hadhi ya Bunge, inayoongozwa na Spika Justin Muturi, imewaalika wabunge hao kufika mbele yake kuangazia madai hayo ambayo yalichipuka baada ya ripoti hiyo iliyoandaliwa na kamati ya pamoja za kilimo na biashara kutupiliwa mbali.
Mnamo Ijumaa Bw Muturi alisema kamati hiyo itaandaa vikao vyake Jumanne na Jumatano ili kupokea ushahidi kutoka kwa wabunge hao, ambao inaaminika wana habari kuhusu madai hayo.
“Mnaalikwa Jumanne na Jumatano kusikiza madai kuhusu iwapo wabunge walipokea hongo au la. Ikiwa kuna mbunge ambaye alidai kuwa aliwaona baadhi ya wenzake akihongwa basi atakuwa fursa siku hiyo kutoa ushahidi au ufafanuzi,” akasema Bw Muturi, akiongeza kuwa vikao hivyo vitakuwa wazi kwa wanahabari.
Miongoni mwa wabunge ambao wameitwa kufika mbele ya kamati hiyo ni; Ayub Savula (Lugari), James Onyango K’Oyoo (Muhoroni), Fatuma Gedi (Mbunge Mwakilishi wa Wajir), Didmas Barasa, na Jane Kihara (Naivasha).
Wengine ni Simba Arati (Dagoretti Kaskazini), Gathoni Wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi wa Kiambu) na Justus Murunga (Matungu).
Wakati wa vikao hivyo, wabunge hao watahitajika kufafanua madai waliyotoa kuwa baadhi ya wenzao walipokea hongo ili kuangusha ripoti hiyo ya kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega na mwenzake wa Mandera Kusini Adan Ali.
Wabunge hao pia watarajiwa kuwasilisha ushahii kuhusu weenzao ambao huenda walipeana au kupokea mlungula wakati huo. Baadaye ushahidi huo, kama utapatikana, utawasilishwa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na asasi zingine husika ili hatua zifaazo zichukuliwe dhidi ya wabunge wahusika.
Duru zinasema kuwa wabunge ambao walinukuliwa na vyombo vya habari wakiwalaumu wenzao kwa kupokea au kupeana pesa hizo watatakiwa kufafanua madai yao.
Miongoni mwao ni Mbw Barasa, Arati, Murunga, Bi Wa Muchomba na Bi Kihara. Bi Wa Muchomb alidai kuwa baadhi ya wabunge walipewa pesa hizo ndani ya vyoo.
Bw Barasa alidai nje na ndani ya bunge kwamba Bi Gedi alijaribu kumhong kwa Sh10,000 zilizokuwa zimewekwa ndani ya bahasha ya zambarau.
Hata hivyo, Bi Gedi amekana madai hayo na kutisha kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Bw Barasa ambaye ni mmoja kai ya wabunge wanne walichaguliwa kwa tiketi ya Jubilee katika kaunti ya Bungoma.
Bw Savula amethibitisha kuwa atafika mbele ya kamati hiyo Jumanne ili kutoa ushahidi alionao.
“Nitafika mbele ya Kamati hiyo Jumanne kwa sababu ni wajibu wetu kurejesha hadhi ya bunge,” akasema Mbunge huyo ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC).
Bw K’Oyoo pia alithibitisha kuwa alikuwa amepokea mwaliko wa kumtaka afike mbele ya kamati hiyo akisema: “Niliitwa kwa sababu mimi ni mwanachama wa kamati hiyo lakin wakati wa mjadala kuhusu ripoti hiyo nilikerwa kwamba haki haikutendewa wakulima wa miwa ambao ninawawakilisha. Kwa hivyo, wamenialika kuwasilisha malalamishi yangu na bila shaka nitafika huko.
Wakati madai hayo yalipoibuliwa, Spika Muturi aliwaalika wapelelezi wa EACC kuchunguza suala hilo.
“Afisi yangu na uongozi wa bunge kwa jumla unachukuwa madai ya hongo katika majengo ya bunge kwa uzito mkubwa. Madai haya yanafaa kuchunguzwa na EACC kwa kina ili hatua za zifaazo zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” akasema.
Kulingana na sheria za bunge, Kamati ya Mamlaka na Hadhi inapaswa kushughulikia masuala kama hayo kabla ya kuyawasilisha kwa asasi kama vile EACC na Idara ya Upelelekezi wa Jinai (DCI).
Ripoti hiyo iliwapata na hatia Waziri wa Fedha Henry Rotich, mwenzake wa Masuala ya Afrika Mashariki Adan Muhammed na Balozi wa Kenya nchini India Willy Bett aliyehudumu kama Waziri wa Kilimo mwaka 2017.