Habari Mseto

Sarafu mpya zitawafaa vipofu – Isaac Mwaura

December 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na IBRAHIM ORUKO

SENETA Maalum Isaac Mwaura amesifia sarafu mpya zilizozinduliwa wiki iliyopita na Benki Kuu ya Kenya (CBK) akisema kuwa zitatambulika kwa urahisi na watu wenye matatizo ya kuona.

Benki ilitoa sarafu hizo kulingana na hitaji la Katiba ya sasa, lililosimamisha matumizi ya picha za marais katika sarafu hizo.

Sarafu mpya zina alama za mimea na wanyama, na zitakuwa zikitumika pamoja na sarafu za sasa.

Sarafu hizo, ambazo zinajumuisha Sh1, Sh5, Sh10 na Sh20 zina miundo inayozifanya kutambulika kwa urahisi na watu wasiokuwa na uwezo wa kuona.

Kiongozi huyo alitaja uzinduzi wa sarafu hizo kama jambo la kihistoria na hatua kubwa itakayohakikisha kwamba watu hao hawatadanganywa tena katika masuala yanayohusu uhesabu wa pesa wanaponunua ama kuuziwa bidhaa.

“Nimefurahishwa sana na sarafu hizo. Uzinduzi wake ni wa kihistoria kwani umeifanya Kenya kujiunga na mataifa machache ambayo muundo wa pesa zake umeshughulikia mahitaji ya watu wasioona,” akasema kwenye taarifa.

Mnamo Septemba, Bw Mwaura aliwasilisha hoja katika Seneti iliyoishinikiza CBK kubuni sarafu zitakazozingatia mahitaji ya watu hao.

Kwenye hoja hiyo, Bw Mwaura alishinikiza uzingatiaji wa mwongozo ambao utatilia maanani mahitaji ya watu hao, akisema kwamba wamekuwa wakiteseka na kudanganywa kwani muundo wa pesa za sasa hauzingatii mahitaji yao.

“Watu hao hawawezi kushiriki katika masuala yoyote yanayohusu uhesabu wa pesa. Hilo limekuwa kikwazo kikubwa kwao katika uendeshaji wa masuala ya kibiashara,” akasema.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) idadi ya watu wasioona imekuwa ikiongezeka nchini.

Kufikia 2016, idadi hiyo iliongezeka hadi 274,000 ambapo kulingana na seneta huyo, wamekuwa wakikumbwa na ugumu kutoa pesa zao katika benki na mashine za ATM.

Bw Mwaura aliwasifia Rais Uhuru Kenyatta na Gavana wa CBK Patrick Njoroge kwa kuzingatia ombi lake.

“Nina furaha kubwa kwani hakuna mtu asiyeona ambaye atadanganywa katika mahali popote panapohusu uhesabu wa pesa,” akasema.