Habari Mseto

Seneta aanza kuhamasisha wakazi Mombasa kuhusu Covid-19

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

SENETA wa Kaunti ya Mombasa Bw Mohamed Faki ameanzisha kampeni madhubuti ya kuhamasisha umma kujua jinsi ya kuepuka maambukizi ya Covid-19 hususan katika vitongoji duni.

Bw Faki ataanza kutembea vitongoji duni akishirikiana na mashirika ya kijamii ili kuhamasisha wakazi dhidi ya ugonjwa huo na namna ya kujikinga.

Amesikitika kwamba wakazi wangali hawana habari madhubuti kuhusu virusi vya corona huku wengi wakichukulia tu kuwa ni homa ya kawaida.

“Kuna changamoto kuhusu virusi vya corona katika makazi ya mabanda lakini kampeni yangu itawahamasisha na watapata mafunzo ya jinsi ya kujikinga,” amesema seneta huyo.

Seneta wa Kaunti ya Mombasa, Bw Mohamed Faki (kati) akizindua kampeni madhubuti ya kuhamasisha umma kuhusu ugonjwa wa Covid-19 ambapo ameweka zingatio katika vitongoji duni. Picha/ Winnie Atieno

Bw Faki alisema kuna habari potovu, itakadi na dhana zinazowakanganya wakazi kuhusu virusi hivyo akisisitiza ipo haja ya wakazi kuhamasishwa vilivyo ili wajikinge kutokana na maradhi hatari ya Covid-19.

Akiongea Jumapili alipozuru baadhi ya vitongoji na kuwafaa wakazi kwa kuwapa barakoa, sabuni na bidhaa zingine za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo, Bw Faki amewataka kudumisha mazingira bora, usafi, kuosha mikono mara kwa mara na kusalia nyumbani ikiwezekana ili kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Seneta wa Kaunti ya Mombasa, Bw Mohamed Faki amsaidia mkazi kuvaa barakoa alipozindua kampeni madhubuti ya kuhamasisha umma kuhusu ugonjwa wa Covid-19 ambapo ameweka zingatio katika vitongoji duni. Picha/ Winnie Atieno

“Ni sharti tufuate maagizo, kanuni na masharti ya Wizara ya Afya ili tujikinge dhidi ya virusi vya corona hususan kwa kuosha mikono kwa kutumia sabuni na maji yanayotiririka, kuvaa barakoa na kukaa nyumbani ikiwezekana,” amesema seneta huyo.

Bw Faki alisema wale wanaoishi sehemu zilizo na wakazi wengi wanaweza kukabiliana na ugonjwa huo endapo watatii maagizo ya wizara.