Seneta ataka magavana wasimamie usalama
Na SHABAN MAKOKHA
SENETA wa Kakamega Cleophas Malala sasa anataka Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuwezesha serikali za kaunti kuhusishwa katika masuala ya usalama.
Bw Malala alisema Katiba ya sasa hairuhusu magavana kujihusisha na masuala ya usalama.
Akizungumza wakati wa kikao cha mashauriano kuhusu usalama, Bw Malala alisema magavana wanastahili kupewa mamlaka ya kukabiliana na visa vya ukosefu wa usalama katika maeneo yao.
Lakini licha ya kutopew mamlaka hayo kwenye Katiba, kuna baadhi ya magavana ambao wanachangia katika udumishaji wa usalama.
Mfano ni Mutahi Kahiga (Nyeri), Hassan Joho (Mombasa) na Alfred Mutua (Machakos) ambao wamenunua magari ambayo yanatumika katika shughuli za usalama.
“Tutashinikiza mabadiliko ya Katiba kwa lengo la kuwezesha magavana kupewa mamlaka ya kudhibiti usalama katika maeneo yao,” akasema Bw Malala.
Seneta huyo pia anataka wananchi wanaojihusisha na masuala ya usalama vijijini na makundi ya Nyumba Kumi wawe wakilipwa mshahara.
Alisema kuhusishwa kwa magavana katika masuala ya usalama kutasaidia pakubwa katika kukabiliana na uhalifu.
Bw Malala alitoa wito huo huku magavana wakishinikiza kuanzishwa kwa mamlaka za kaunti za kukabiliana na masuala ya usalama.
Juhudi za magavana kutaka kuhusishwa katika masuala ya usalama hazijazaa matunda licha ya kukutana mara kadhaa na Waziri wa Usalama na maafisa wakuu wa polisi.
Mamlaka ya usalama katika kaunti ilichapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali mnamo Januari 2015 lakini kufikia sasa hazijaanza kufanya kazi kwani serikali ya kitaifa imeshikilia kuwa usalama ni jukumu lake na haujagatuliwa.
Mnamo 2016, Rais Uhuru Kenyatta alikutana na magavana katika Ikulu ya Nairobi, ambapo waliafikiana kuwa mamlaka hizo zitaanza kufanya kazi. Katika mkutano huo, magavana walikubali watakuwa wakiripoti kwa serikali ya kitaifa kuhusu hali ya usalama katika maeneo yao kila baada ya wiki mbili. Lakini hakuna hatua zilizopigwa kufikia sasa.
Mamlaka ya Usalama katika Kaunti ilibuniwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Polisi na lengo lake kuu lilikuwa kuboresha usalama katika kaunti.
Kifungu cha 41 cha sheria hiyo kinasema kuwa mamlaka hiyo itasimamiwa na gavana au waziri wa kaunti atakayeteuliwa na gavana.
Bw Malala alisema kuwa mamalaka hizo zitasaidia pakubwa katika kuhakikisha kuwa visa vya ukosefu wa usalama vinakabiliwa katika kaunti.