Seneta Mkenya ajipata kwa kashfa ya pesa Australia
Na VALENTINE OBARA
SENETA wa Jimbo la Australia Kusini ambaye ni mzaliwa wa Kenya, Bi Lucy Gichuhi, amehusishwa na kashfa ya utumizi mbaya wa pesa za umma kwa manufaa ya kibinafsi.
Ilifichuliwa kwamba Bi Gichuhi alitumia pesa za umma kusafirisha jamaa zake wawili kuhudhuria karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake.
Seneta huyo jana alikiri ripoti hizo ni za kweli, lakini akajitetea kuwa hali hiyo ilitokana na makosa ya usimamizi na tayari ameanzisha mipango ya kurudisha Sh213,900 zilizotumika.
“Kufuatia ripoti za vyombo vya habari kuhusu gharama zangu za usafiri, hii ilikuwa ni makosa ya kiusimamizi iliyotokana na kutoelewa sheria za usafiri,” akasema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.
Mashirika ya habari yalikuwa yameripoti kuwa pesa hizo zilitumiwa kusafirisha jamaa hao wa familia yake hadi Adelaide, ambao ni mji mkuu wa Australia Kusini, ingawa haikubainika wazi walisafiri kutoka wapi.
Kulingana na sheria za bunge la Australia kuhusu usafiri, wabunge na maseneta huruhusiwa kupokea marupurupu ya usafiri wa jamaa zao kama safari zao ni za kikazi hasa ikiwa ni za muda mrefu.
Marupurupu hayo hayanuiwi kufadhili safari za kibinafsi, kwa mujibu wa mashirika ya habari nchini humo.
Bi Gichuhi, 56, alipata umaarufu humu nchini aliposhinda wadhifa huo kwani aliingia kwenye orodha ya Wakenya wanaofanya makuu kimataifa. Ushindi wake uliibua mdahalo kwamba huenda akafuata nyayo za aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama ambaye babake alikuwa Mkenya.
Mzaliwa huyo wa Kenya alihamia Australia katika mwaka wa 1999 pamoja na mumewe na watoto ambapo alifanya kazi za uhasibu na uwakili kabla kujitosa katika siasa.
Pingamizi kuhusu ushindi wake liliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Australia kwa madai kwamba alikuwa angali ni raia wa Kenya lakini mahakama ikapata hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha bado anashikilia uraia wake wa Kenya.
Sheria za nchi hiyo zinasema mtu aliye na uraia wa mataifa mawili haruhusiwi kushikilia wadhifa wa uongozi wa kisiasa.