Seneta Mutula Jr alazwa hospitalini baada ya kusakamwa na nyama ya kuku
TOM MATOKE na BENSON MATHEKA
SENETA wa Kaunti ya Makueni Mutula Kilonzo Junior, Jumatano alikimbizwa hospitalini baada ya kusakamwa na kipande cha nyama ya kuku akiwa katika Kaunti ya Nandi.
Hata hivyo, alikanusha kwamba alizirai kufuatia kisa hicho ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na kusambaza mitandaoni.
Kupitia ujumbe wa Twitter, seneta huyo aliwaondolea hofu wakazi wa Makueni na Wakenya kwa jumula alipotangaza kuwa alikuwa buheri wa afya. “ Niko salama na sikuzirai,” aliandika Bw Kilonzo baada ya habari kuenea mtandaoni kwamba alikuwa amezirai.
Hata hivyo, alikiri kwamba alikuwa amesakamwa koo wakati akila chakula cha mchana.
Afisa Mkuu wa Hospitali ya Moi Teaching and Referral, Dkt Wilson Aruasa, alithibitisha kuwa Seneta huyo alikuwa amesakamwa na kipande cha nyama ya kuku ambacho kilitolewa na madaktari.
“Baada ya kutolewa katika hospitali ya Kapsabet, ambapo alipata huduma ya kwanza, tulimpeleka katika chumba cha upasuaji hapa Moi na baada ya uchunguzi tukagundua kipande kidogo cha nyama ya kuku ambacho kimetolewa lakini atalazwa hadi kesho ili apate matibabu ya kutosha,” alisema Dkt Aruasa.
Seneta wa Nandi Samson Cherargei pia alithibitisha kuwa Seneta Kilonzo hakuzirai. “Seneta Mutula hakuzirai lakini alisakamwa tulipokuwa tukila chakula katika hoteli ya Eden baada yangu kuhutubia bunge la Kaunti ya Nandi. Kwa sasa anapokea matibabu,” Bw Cherargei aliandika kwenye Twitter.
Habari zilikuwa zimeenea kwamba seneta huyo alianguka na kuzirai baada ya kusakamwa na kipande cha nyama akiwa katika hoteli ya Eden Springs mjini Kapsabet.
Alikuwa ameandamana na maseneta wengine Yusuf Haji, Mohamed Faki, Rose Nyamunga, Boniface Kabaka, Juma Boy, Kinyua Nderitu na Stewart Madzayo kutembelea bunge la Kaunti ya Nandi.
Seneta Kilonzo alipelekwa katika hospitali ya Kaunti ya Kapsabet kwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa hospitali ya rufaa ya Moi mjini Eldoret ambako madaktari walisema hakuwa hatarini.
Habari kwamba alikuwa amezirai zilishtua Wakenya waliomtakia afueni ya haraka kupitia jumbe mtandaoni.
“Tunafurahi kusikia uko sawa, tulikuwa tumeshtuka,” aliandika Peter Amiga kwenye Twitter.
Diwani mteule wa bunge la Kaunti ya Makueni, Mbula Mutula aliandika kwenye Facebook: “Seneta wa Makueni aliye gavana mtarajiwa Mutula Kilonzo Jr yuko sawa. Alisakamwa na chakula tu lakini yuko sawa na tunashukuru Mungu. Tunamtakia mema. Asanteni marafiki kwa maombi yenu.”