Habari Mseto

Seneti yapitisha mswada wa Wakenya kuendelea kulipa ushuru wa nyumba

March 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

COLLINS OMULO Na CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amepata ushindi katika mpango wa serikali yake kuendelea kuwatoza Wakenya ushuru wa nyumba baada ya maseneta wa Kenya Kwanza kulemaza jududi za wenzao wa Azimio kuufanyia marekebisho Mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu (AHB).

Maseneta hao waliangusha marekebisho kwa mswada huo yaliyopendekezwa upande wa Azimio na uliolenga kutoa afueni kwa Wakenya kwa kuwapunguzia mzigo wa ulipaji wa ushuru huo.

Kwenye kikao cha Seneti cha Jumanne jioni ambako mswada wa AHB ulishughulikiwa kwa awamu ya tatu, Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni alikuwa amependekeza makato ya juu zaidi ya ushuru huo kwa mapato ya Wakenya kila mwenye yawe Sh2,500.

Aidha, Seneta huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM alitaka ushuru huo wa kima cha asilimia 1.5 utozwe mishahara ya kimsingi ya wafanyakazi wala sio mapato ya jumla, yakiwemo marupurupu.

Kulingana na mswada huo ambao tayari umepitishwa katika Bunge la Kitaifa, ushuru huo wa asilimia 1.5 unatozwa kwa jumla ya mshahara wa mfanyakazi kila mwezi au mapato ya jumla ya Mkenya yeyote kwa kipindi hicho.

Bw Omogeni pia alitaka Waziri wa Fedha kuwasaza dhidi ya kulipa ushuru huo, mtu yeyote ambaye analipia mkopo wa nyumba aliouchukua kabla ya kuanzishwa kwa ushuru huo, watu wanaoishi mashambani na wanamiliki ardhi na mtu yeyote anayeendesha shughuli za kilimo au biashara na ambaye mapato yake kila mwaka hayazidi Sh288,000.

Lakini kura ilipopigwa kuhusu marekebisho hayo, jumla ya maseneta 27 wa Kenya Kwanza walipa kura ya NDIO kudumisha mswada huo ulivyopitishwa katika Bunge la Kitaifa mwezi jana. Nao jumla ya maseneta 10 wa upinzani waliunga mkono mapendekezo hayo ya mwenzao Seneta Omogeni

Hata hivyo, maseneta wengine 10 wa mrengo wa Azimio hakuwepo ukumbini wakati wa shughuli hiyo ya upigaji kura uliosimamiwa na Naibu Spika Kathuri Murungi.

“Matokeo ya upigaji kura wa moja kwa moja ni kama yafuatayo, hamna waliosusia, waliopiga kura ya NDIO ni 27 na waliopiga kura ya LA ni 10. Upande wa NDIO imeshinda. Kwa hivyo, baada ya kukamilishwa kwa shughuli zilizoorodheshwa na wakati huu ambapo zinasalia dakika tano kabla ya saa moja za usiku, bunge hili limeahirishwa hadi kesho (Jumatano),” akasema Bw Murungi ambaye ni Seneta wa Meru.

Hiyo ina maana kuwa sasa Rais Ruto anasubiriwa kuutia saini mswada huo ili uwe sheria.

Seneta Omogeni pia alikuwa amependekeza kuwa watu wenye umri wa miaka 50 kwenda juu na wanaendesha biashara ndogo ndogo na watu ambapo wamesalia na miaka mitano kabla ya kustaafu wasazwe kulipa ushuru wa nyumba.

Aidha, Seneta huyo wa Nyamira alipendekeza kuwa pesa zitakazokusanya kupitia ushuru huo wa nyumba zitengewe serikali za kaunti kama ruzuku ya miradi maalum, ili zisimamie matumizi ya fedha hizo.

Kulingana na mswada huo wa Nyumba za Gharama Nafuu fedha zinazokusanywa kutokana na ushuru huo zitasimamiwa na Bodi ya Hazina ya Nyumba.

“Wajibu wa ujenzi wa nyumba ni wa serikali za kaunti kulingana na Mpangilio wa Nne wa Katiba. Ikiwa wajibu huu utatwikwa wajibu huu basi hiyo itakuwa ni kinyume cha Katiba,” akasema Bw Omogeni.

Hata hiyo pendekezo lililowasilishwa na Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wa kwamba mtu mmoja aliyetimiza masharti yote ya kununua nyumba hizo aruhusiwe kununua nyumba moja pekee lilipitishwa.

Aidha, Seneta huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uchukuzi alipendekeza kuwa aliyenunua nyumba chini ya mpango huo azimwe kuuza nyumba hiyo kwa mtu mwingine.

Baada ya Rais Ruto kuutia saini mswada huo, Wakenya walioajiriw ana wale waliojiari wataendelea kulipa ushuru wa nyumba wa kima cha asilimia 1.5 ya mapato yao kila mwezi.

Ulipaji wa ushuru huo ulisitishwa na mahakama kuu mnamo kwa misingi kuwa ulikuwa haramu kwa kuwabagua watu walioajiriwa na kuwasaza wale ambao wamejiari au wanaendesha biashara