Serikali itangaze kansa janga la kitaifa – Wabunge
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wanaitaka serikali ya kitaifa kutangaza kansa kuwa janga la kitaifa na ibuni hazina maalum ya kufadhili matibabu ya ugonjwa huo hatari.
Jumatano, wabunge hao ambao walikuwa wakichangia hoja iliyodhaminiwa na Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Cathrine Waruguru walisema kuwa gharama ya kutibu ugonjwa huo ni juu kiasi kwamba Wakenye wengi hawawezi kuimudu.
Akianzisha mjadala kuhusu hoja hiyo Bi Waruguru alisema Wakenya hawatafariki kwa wingi, ilivyo sasa, ikiwa serikali itatangaza kansa kuwa janga la kitaifa. Hii, akasema, ni kwa sababu hatua hiyo itapelekea wahisani wengi kutoka humu nchini na ng’ambo kuwekeza rasilimali nyingi katika mipango ya kuudhibiti.
“Tunawajali wagonjwa wanaougua kansa na ndi maana nimechukua hatua hii inayolenga kuwapunguzia matesa. Ugonjwa huu ukitangazwa kuwa janga la kitaifa watu wengi wataweza kuhamasishwa juu yake na wahisani wengi watajitokeza kusaidia kufadhili matibabu na mikakati ya kuudhiti,” akasema Bi Waruguru.
Akaongeza: “Wakenya wengi masikini wanaendelea kuteseka kwa kukosa fedha za kugharamia matatibu. Hii ni kwa sababu Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) na ile ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH),ambazo ndizo za kipekee zinazotibu kansa nchini, hazina vifaa na wataalamu wa kutosha,”.
Wabunge walisema hospitali za kibinafsi kama vile Nairobi Hospitali, Aga Khan na MP Shah mbazo zina vifaa vya kisiasa na wataalamu wa kutoka ni ghali mnamo na raia wa kawaida hawawezi kumudu.
Mbunge wa Nyatike Tom Odege alisema utepetevu wa serikali katika kupambana na kansa ndio hupelekea watu wengi kufariki kutokana na ugonjwa huu.
“Mbona matibabu ya kansa ni nafuu nchini India kuliko humu nchini Kenya ilhali gharama hiyo inajumuisha nauli ya ndege na malazi? akauliza.
Mbunge huyo wa chama cha ODM alisema kuna uwezekano mkubwa mgonjwa kufariki akisubiri matibabu katika hospitali ya KNH na MTRH kwa sababu ya uhaba wa vifaa na madaktari.
Mbunge Maalum Bi Cecily Mbarire aliitaka serikali kuanzisha kampeni ya kutoa uhamasisho kuhusu kansa kama ilivyofanya kuhusu Ukimwi na virusi vya HIV ili Wakenya waweze kupata ufahamu kuhusu kansa.
Uhamasisho
“Wakenya wanafaa kufundishwa kuhusu umuhimu wa kukaguliwa mapema kubaini ikiwa wanaugua kansa,” akasema.
Naye Mbunge wa Seme Dkt James Nyikali aliitaka serikali kufungua vituo vya kukugua kansa kuanzia mazahanati hadi hospitali ya mijini.
“Ikiwa kutabuniwa vituo vya kukagua kansa katika maeneo ya mashinani, kwenye mazahanati bila shaka ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa mapema kabla ya kuenea na kuwa sugu,”akasema mbunge huyo ambaye ni daktari wa tiba ya binadamu.
Mbunge huyo pia alitoa wito kwa umma kuepukana na vyakula vilivyotengenezwa viwandani akisema ndio huwa na kemikali zinazosababisha kanza.
Kulingana na takwimu kutoka Wizara ya Afya takriban watu 28,000 hufariki nchini kila mwaka kutokana na kansa huku jumla ya watu 2.8 milioni wakiangamizwa na ugonjwa duniani kila mwaka.
Wabunge hao pia waliitaka serikali za kaunti kuweka vifaa vya kisasa na dawa katika hospitali za umma ili kusaidia kudhibiti ugonjwa huu hatari.