Serikali kuchukua data ya DNA ya Wakenya kwenye usajili mpya
Na MOHAMED AHMED na BONIFACE OTIENO
WAKENYA wote sasa watasajiliwa upya katika sajili ya kidijitali na kupewa nambari maalum ambazo zitakuwa na maelezo ya mtu binafsi, Rais Uhuru Kenyatta ametangaza.
Tangazo hilo limetolewa siku chache baada ya rais kuidhinisha marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Watu na kufanya wale wanaojiandikisha kutaka vitambulisho watoe habari zaidi ikiwemo DNA.
Katika sheria hiyo, serikali inataka pia kuanza kutumia teknolojia ya setilaiti kutambua mahali halisi watu wanakoishi.
Katika utambulisho wa kibinafsi, serikali imeongeza masharti ya kujiandikisha ili kujumuisha DNA za wanaojisajili kwa njia za dijitali, sauti zao na muundo wa ndewe za masikio yao.
“Kuandikisha data za sehemu za mwili… inamaanisha utambuzi maalumu ikiwemo alama za vidole, miundo ya mkono, ndewe ya sikio, mboni na retina ya macho, sauti na DNA kidijitali,” sehemu ya sheria hiyo inasema.
Awali serikali ilihitaji tu alama za vidole vya mkononi au mguu.
Sheria hiyo mpya inawezesha uundaji wa rekodi maalumu ya kitaifa ambayo itahakikisha usajili wote wa vitambulisho, kadi za wakimbizi, vyeti vya kuzaliwa au kufa na leseni za uendeshaji magari unafanywa mahali pamoja kwenye mtandao mmoja almaarufu kama NIMS.
Akizungumza Mombasa jana katika kikao na maafisa wa usalama wakiwemo makamishna na makamanda wa polisi, Rais Kenyatta alisema nambari maalumu zitakazotambulika kama “Huduma Namba” zitapeanwa baada ya kukamlika kwa mpango huo mpya wa usajili.
“Katika kila usajili ambao utafanywa na mtandao wa NIMS kutapeanwa nambari hiyo ambayo itajulikana kama ‘Huduma Namba’,” akasema rais.
Alisema mpango huo unapania kuupa jeki mtandao wa Integrated Population Registration System (IPRS) uliozinduliwa 2015 na unaotazamiwa kuweka taarifa za watu zilizoko katika afisi tofauti za serikali pamoja ili kuimarisha usalama na utendakazi.
Data hiyo pia itaweka mahala moja taarifa za Wakenya na wageni ili kurahisisha kupatikana kwazo zinapohitajika.
Miongoni mwa maelezo yatakayokuwa kwenye sajili hiyo ni pamoja na maelezo yanayopatikana katika afisi kama vile za vyeti vya kuzaliwa na vifo, ndoa na talaka pamoja na pasi ya usafiri na vitambulisho.
Taarifa kama hizo zitawekwa pamoja na kuwezesha afisi kama vile za ardhi, bima ya afya, vyuo vikuu na IEBC kuweza kupata taarifa za mtu binafsi kwa urahisi.
Vile vile, data hiyo itawezesha IEBC kuzuia wapiga kura kutumia vitambulisho vya waliokufa.
Tangazo la jana la Rais Kenyatta lilitolewa siku moja baada ya waziri wa masuala ya ndani Fred Matiang’i kuelekeza kuwa raia wote wanaomiliki bunduki wapate kadi za kidijitali ifikapo Machi 19.
Dkt Matiang’i mnamo Jumatatu alisema kuwa kadi hizo zitakuwa na maelezo ya kila anayemiliki bunduki na atatakiwa kuonyesha iwapo ataulizwa na afisa husika.
Alisema kuwa hilo lililenga kupambana na uhalifu ambao umehusisha utumizi wa bunduki humu nchini.