Serikali kudukua simu za wanahabari wanaoikosoa
NA MWANDISHI WETU
JE, una mazoea ya kutumia simu kukashifu serikali, kufichua maovu na kutuma jumbe za kibinafsi ukidhani ni siri kubwa?
Kama ni kweli basi unafaa uchukue tahadhari kwani serikali sasa ina uwezo wa kufuatilia kila unachofanya kwenye simu yako ama hata mahali ulipo.
Hii ni baada ya kufichuka kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa 30 ambayo yanatumia teknolojia ya kudukua mawasiliano ya simu za raia hasa wanahabari na watetezi wa haki za binadamu.
Kulingana na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, mataifa mengi ambayo yanatumia teknolojia hiyo maarufu kama Pegasus kutoka kwa kampuni NSO Group ya Israeli, yana rekodi ya ukiukaji wa haki za binadamu na utawala wa kidikteta.
Mataifa ambayo pamoja na Kenya yametajwa kuingilia simu za raia wake ni Saudi Arabia, Rwanda, Uganda, India, Mexizo, Qatar na Bahrain miongoni mwa mengine.
Lakini kampuni ya NSO Group imejitetea kuwa teknolojia yake inakusudia kusaidia mashirika ya usalama na ujasusi kuzuia na kupeleleza visa vya uhalifu kama vile ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi ili kulinda maisha ya watu kote duniani.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa shirika la The Citizen Lab lenye makao yake nchini Canada, Ron Deibert anasema katika uchunguzi wao wamegundua kwamba nia kuu ya serikali zinazotumia Pegasus ni kuzima wakosoaji wao na utoaji wa habari kuhusu maovu ndani ya serikali zao.
“Hii ni teknolojia maarufu kwa serikali ambazo haziheshimu haki za binadamu na za kidikteta. Kwa mfano tumefuatilia matumizi yake nchini Rwanda na inaonyesha inatumiwa katika kuwadhulumu wakosoaji wa serikali,” akasema Bw Deibert.
Kulingana na utafiti wa Al Jazeera, wanahabari na watetezi wa haki za binadamu ndio walengwa wakuu wa udukuzi wa simu.
Bw Deibert alieleza kuwa teknolojia hii ni rahisi sana kupenya kwenye simu za wanaolengwa kwani inabidi tu kupigia mtu simu pekee na hata kama hatachukua utakuwa tayari umepenye kwenye simu yake.
Pia mtandao wa WhatsApp unatumiwa hasa ule wa kupiga simu kwa video.
“Ukishapenya kwenye simu unapata habari zote za mhusika, jumbe anazotuma, simu anazopiga, anayosema ama kuandika kwenye mitandao ya kijamii, kamera yake na kila mahala anakoenda kupitia GPS. Hii ni hatari sana kwa wanahabari na wakosoaji wa serikali,” akasema Bw Deibert.
Tayari wanahabari na watetezi haki za binadamu nchini India na Saudi Arabia wameripoti kupokea jumbe za vitisho ambazo The Citizen Lab inasema zinatumwa na maafisa wa serikali.
Tayari WhatsApp imewasilisha kesi mahakamani kulalamikia tekinolojia hiyo ambayo inasema inatishia uhuru wa kibinafsi wa wateja wake.
Hatua hiyo ya serikali ya kudukua habari kwa kusikiza mawasiliano ya watu, ilipingwa miaka miwili iliyopita, ambapo baadhi ya wanaharakati walitishia kuzishtaki kampuni za mawasiliano nchini, kama zingethubutu kurruhusu mitandao yao itumiwe vibaya na serikali.