Serikali kujenga daraja kuu kukabili ongezeko la maafa
NA BONIFACE MWANIKI
Serikali kuu kupitia Wizara ya Uchukuzi, imeahidi kujenga daraja kwenye Mto Enziu, katika barabara inayounganisha eneo la Nguni na Nuu, kaunti ya Kitui.
Hii ni kufuatia maafa mengi yanayoshuhudiwa katika mto huo wakati wa mvua kubwa.
Mto huo umeripotiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 10 tangu Julai mwaka uliopita.
Mwaka jana, Mto Enziu ulipata umaarufu wa aina yake baada ya mafuriko kusomba gari aina ya Toyota Probox na kuwaua watu wanne waliokuwa wakielekea upande wa Nuu. Ilichukua zaidi ya wiki tatu kuopos miili ya wanne hao kutoka kwenye mto huo.
Mbunge wa zamani wa eneombunge ya Mwingi ya Kati Bwana Joe Mutambu alifanya jaribio la kujenga daraja kwenye mto huo akitumia hazina ya CDF, lakini juhudi zake ziliambulia patupu.
Na hatimaye kuna matumaini baada ya serikali kutoa ahadi kwa wakazi kupitia kwa Katibu wa Wizara ya Ujenzi Paul Maringa kuwa, itajenga daraja katika eneo hilo haraka iwezekanavyo.
Akizungumza alipozuru eneo hilo mnamo Ijumaa, Bw Maringa alisema Serikali ilikuwa makini kuzingatia usalama wa Wakenya na kwa hivyo itajenga daraja lenye upana wa mita 100 katika mto Enziu ili kuzuia maafa zaidi.
“Ningependa kusema kuwa serikali yetu inajali usalama wa kila Mkenya, na hatuwezi kufurahia mnapoteseka. Hivyo, serikali kuu kupitia wizara ya Ujenzi itajenga daraja kwenye mto huu ili kuhakikisha hakuna Mkenya mwingine atapoteza maisha yake katika eneo hili kwa kusombwa na maji,” aliahidi Bw Maringa.
Alisema kama hatua ya dharura, serikali itarekebisha daraja la zamani kwenye mto huo, ili kuwezesha usafiri wakati hakuna mvua, huku juhudi za kutengeneza daraja kubwa linalopita juu ya mto zikiendelea.
Akizungumza katika eneo hilo, Mbunge wa Mwingi ya Kati aliyeandamana na katibu huyo Dkt Gideon Mulyungi alitoa shukrani kubwa kwa serikali kuu chini ya utawala wake Rais Uhuru Kenyatta kwa kukubali kujenga daraja hilo.