Habari Mseto

Serikali kutumia Sh1.9 bilioni kununua madawati maalum

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

WIZARA ya Elimu itatumia Sh1.9 bilioni kununua madawati maalum kwa wanafunzi wa shule za msingi na upili nchini huku shule zikitarajiwa kufunguliwa.

Waziri wa Elimu George Magoha amesema serikali inajizatiti kuhakikisha usalama wa wanafunzi kabla ya kufunguliwa kwa shule.

Akiongea wakati wa ziara alizofanya katika chuo kikuu cha Mombasa na kile cha Pwani kilichoko Kilifi, Bw Magoha amesema makamishna wa kaunti 47 nchini watasimamia mfumo wa madawati hayo ili kuhakikisha yanawiana na masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Shule zilifungwa mnamo Machi 20, 2020, tangu wakati huo Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitusisitizia umuhimu wa kuhakikisha tunafuata taratibu na usalama wa wanafunzi wote. Alisema ni sharti shule za chekechea, msingi, upili na vyuo vikuu vifuate masharti ya Covid-19,” alisema Prof Magoha.

Alisema madawati hayo yataundwa na sekta ya juakali zilizoko wilayani kabla ufunguzi wa shule.

Akiongea alipoenda kuthmini matayarisho ya ufunguzi wa vyuo vikuu vya Pwani na Mombasa, Prof Magoha alisema fedha za madawati ziko tayari kufuatia agizo la Rais Kenyatta.

Prof Magoha alisema wanathmini virusi vya corona kwa kipindi cha wiki mbili kabla ya kutoa maamuzi kuhusu ufunguzi wa shule.

Alisema vyuo vikuu vilitarajiwa kufunguliwa mwezi huu wa Septemba lakini mpango huo ukasitishwa kufuatia matayarisho mabaya na kuongezeka kwa visa vya corona nchini.

Alisisitiza kuwa taasisi zote za elimu lazima ziwe salama kabla ya kufunguliwa ikiwemo kuhakikisha kuna sehemu ya kuosha mikono na kufuata masharti ya serikali kuhusu Covid-19.