Serikali kuu kusimamia Nairobi hadi 2022
Na JAMES KAHONGEH
MAELEWANO kati ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Serikali Kuu kuhusu usimamizi wa kaunti hiyo yamepangiwa kuanza kutekelezwa Machi 15.
Makubaliano hayo yatadumu kwa miezi 24, kisha upande wowote husika, kati ya Serikali Kuu na ya kaunti utaamua ikiwa utaongezwa muda.
Kipindi hicho kinamaanisha kwamba, majukumu ya kusimamia afya, uchukuzi, ujenzi na mipango ya kaunti yatakuwa chini ya Serikali Kuu hadi Februari 25, 2022. Hii ni kumaanisha mkataba utakamilika miezi michache kabla Uchaguzi Mkuu kufanyika.
Kwa msingi huu, endapo Bw Sonko atang’olewa mamlakani, huenda atakayechukua nafasi yake asiwe na majukumu makubwa kwani idara hizo nne ni miongoni mwa kubwa zaidi za kaunti.
Kinachoshangaza ni kuwa, Serikali Kuu itachukua pia jukumu la kukusanya na kugawa mapato yote yanayopatikana katika idara hizo kupitia kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kitaifa (KRA).
Kwa mujibu wa nakala iliyotiwa sahihi na Bw Sonko na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumanne, makubaliano hayo hayawezi kukatizwa na upande wowote kabla muda ulioekwa kukamilika isipokuwa kama pande zote mbili zitakubali kufanya hivyo.
Hata hivyo, imebainika makubaliano hayo yatahitaji kufanyiwa utathmini na bunge la kaunti kabla kutekelezwa, imefichuka.
Vilevile, wananchi watapewa muda kuwasilisha maoni yao kuhusu mpango huo wa kukabidhi utawala wa Rais Uhuru Kenyatta sehemu ya usimamizi wa jiji hilo kuu la Kenya.
Majukumu yaliyopeanwa kwa Serikali Kuu yatafadhiliwa na fedha kutoka kwa Hazina ya Mapato ya Kaunti au Hazina ya Jumla au zote mbili.
Hii ni kutokana na kuwa, Serikali ya Kaunti ya Nairobi itahitajika kufadhili idara hizo nne kikamilifu.
Maelewano mengine ni kwamba, Kaunti ya Nairobi itahitajika kupeana wafanyakazi kwa serikali kuu ili kufanikisha utekelezaji wa maelewano hayo.