Serikali kuwasaidia vijana kuajiriwa ng'ambo – Yatani
Na ANTHONY KITIMO
SERIKALI kwa ushirikiano na sekta ya kibinafsi zimeweka mikakati kabambe ya kuwatafutia vijana kazi katika mataifa ya ng’ambo.
Waziri wa Leba ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Fedha, Ukur Yatani, alisema serikali imepiga msasa maajenti na kuweka mipango ya kusafirisha vijana wote wanaopata ujuzi katika vyuo vya ufundi anuwai nchini kufanya kazi ng’ambo.
Bw Yatani alisema serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha vijana wote wanapata ujuzi na vyeti ambavyo vinakubalika kote duniani.
“Serikali inajali maslahi ya vijana ndio maana inawekeza katika vyuo vya ufundi na kuwapa fedha za kujikimu wakati wa masomo yao lakini tunawapa changamoto viongozi katika kaunti zote nchini waweze kuunga mkono serikali kuu kwa kutenga fedha za kusaidia vijana kujiunga na vyuo hivyo,” alisema waziri huyo.
Akiongeza mjini Mombasa baada ya kuzindua karakana za kisasa katika National Industrial Training Authority (NITA), zilizojengwa kwa msaada kutoka serikali ya Korea kwa gharama ya zaidi ya Sh300 milioni, Bw Yatani alisema wanawasiliana na maafisa wa serikali katika nchi mbali mbali kuunganisha vijana waliopata ujuzi mbalimbali wapate ajira katika nchi hizo.
Baadhi ya nchi ambazo serikali inanuia kupeleka vijana kufanya kazi mbalimbali ni pamoja na Qatar, Saudi Arabia na Milki ya Uarabuni (UAE).
Serikali tayari imepiga msasa baadhi ya maajenti wanaojihusisha na kupeleka vijana nchi mbalimbali kutafuta ajira ili kupunguza visa vya unyanyasaji wanapofika katika nchi hizo.
Miaka mitatu iliyopita, serikali iliondoa marufuku ya kupeleka Wakenya nchi za ng’ambo kufuatia kuongezeka kwa visa vya unyanyasaji baada ya kuweka mikakati ya kupunguza visa hivyo.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 4 milioni hufanya kazi mbalimbali ng’ambo na ikiwa mikakati maalumu itawekwa, idadi hiyo inaweza kuongezeka maradufu na kupunguza changamoto ya uhaba wa kazi nchini.