Habari Mseto

Serikali sasa yaahirisha KCPE na KCSE hadi 2021

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na WANDERI KAMAU

MITIHANI ya kitaifa haitaandaliwa mwaka huu baada ya kuahirishwa hadi mwaka ujao kwa sababu ya janga la corona, serikali imethibitisha.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema kuna uwezekano mkubwa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) na ule wa Shule za Upili (KCSE) kufanywa Aprili mwaka ujao.

Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ameagiza wizara hiyo ishauriane na wadau kuhusu jinsi shule zitakavyofunguliwa kuanzia Septemba mwaka huu.

“Kama shule zitafunguliwa Septemba, mwezi Aprili ndio wakati mwafaka wa watahiniwa kufanya mitihani ya kitaifa,” akasema jana alipofika mbele ya kamati ya muda ya seneti kuhusu janga la Covid-19.

Alisema kamati iliyoundwa kujadili ufunguzi wa shule itatoa mwelekeo wiki mbili zijazo kuhusu kama itawezekana kufungua shule Septemba.

“Mitihani ya kitaifa sharti ifanywe Aprili mwaka ujao, kwa sababu watahiniwa na walimu watahitaji muda wa kutosha kujiandaa,” akaambia kamati hiyo inayooongozwa na Seneta wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja.

Mitihani ya KCPE na KCSE ilikuwa imeratibiwa kuanza Oktoba mwaka huu hadi mwishoni mwa Novemba kabla ya mlipuko wa Covid-19 kuvuruga ratiba ya masomo.

Endapo mitihani hiyo itafanywa mwaka ujao, kuna uwezekano mkubwa kuwa ratiba nzima ya shule itabadilika.

Huenda ratiba mpya kuelekea mbele itahitaji muhula wa kwanza uwe ukianzia katikati ya mwaka badala ya Januari jinsi ilivyokuwa desturi humu nchini kabla ya corona.

Wakati huo huo, Wizara ya Elimu imetoa ilani kwa wasimamizi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kuanza maandalizi ya kuzifungua. Kwenye notisi maalum kwa wakuu wa vyuo jana, Katibu katika Idara ya Elimu ya Vyuo Vikuu na Utafiti, Bw Simon Nabukwesi, alisema vyuo vinavyotumika kama karantini viache kuchukua watu zaidi walioambukizwa corona, na badala yake kuweka mikakati ya kurejelea shughuli zake za kawaida.

Alisema kuwa taasisi zinapaswa kushirikiana na Wizara ya Afya kuwaelekeza watu hao kwenye vituo vingine.

Vyuo pia vilitakiwa kuyanyunyizia dawa ya kuua vini majengo ambayo yamekuwa yakitumika kuwaweka watu hao.

Wakuu pia wanatakiwa kutayarisha ripoti kuhusu mikakati waliyoweka na kuzituma kwa wizara husika kufikia Juni 25.

Katibu huyo pia aliviagiza kuweka juhudi kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi amerejea vyuoni, pindi vitakapotangaza kurejelea upya shughuli zake za kawaida.

Serikali ilitangaza kuwa shughuli za kawaida za masomo zitaanza kurejelewa kuanzia Septemba 1, baada ya kasi ya maambukizi ya virusi kupungua.