Habari Mseto

Serikali yakataa kulegeza kanuni za kafyu mwezi wa Ramadhan

April 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na IBRAHIM ORUKO

SERIKALI imekataa ombi la viongozi wa Waislamu la kutaka Wizara ya Afya ilegeze sheria za kafyu mwezi mtukufu wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza wiki hii.

Hii ni baada ya Imamu kuaga dunia kutokana na virusi vya corona mtaani Eastleigh, Nairobi wiki jana.

Badala yake, Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, aliwataka viongozi hao wahakikishe sheria hiyo ya kafyu inazingatiwa vilivyo katika maeneo yao wakati wa mwezi huo muhimu wa kidini.

Bw Kagwe alisema, baadhi ya viongozi wa makanisa pia wamekuwa wakipuuza mikakati iliyowekwa na wizara yake kukabiliana na virusi hivyo ndiyo maana kafyu hiyo haiwezi kulegezwa kamwe.

“Hatutalegeza kafyu hata baada ya kupokea ombi la viongozi wa kidini, wakiwemo Waislamu. Viongozi wa kidini ndio wanafaa wawe mstari wa mbele kuhakikisha mikakati iliyowekwa inatekelezwa kikamilifu,” akasema Bw Kagwe alipofika mbele ya kamati ya Bunge la Seneti inayoangazia janga la virusi vya corona.

Kamati hiyo iliandaa kikao na Waziri huyo kwa njia ya mtandaoni na ilikuwa mara ya kwanza mkutano kama huo ulikuwa ukiandaliwa na Bw Kagwe aliyeteuliwa kuhudumu kwenye wizara hiyo hivi majuzi.

Mnamo Ijumaa wiki jana, Baraza Kuu la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) liliomba serikali isongeshe muda wa kafyu kutoka saa moja jioni hadi saa nne usiku ili kuwaruhusu Waislamu wazingatie vyema mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Waislamu hutumia muda huo baada ya kufungua kugawa vyakula au kula pamoja na watu wasiojiweza katika jamii. Vile vile, walitaka misikiti ifunguliwe, wakiahidi kufuata kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Katika kikao cha Seneti, suala hilo liliibuliwa na Seneta wa Mombasa Mohamed Faki, ambaye pia ni mwanachama wa kamati hiyo. Bw Faki alimwomba Waziri Kagwe alegeze sheria za kafyu, akimhakikishia kwamba, Waislamu watazingatia viwango vya juu vya usafi na mikakati kuhusu kukaa umbali wa mita moja unusu.

“Tutaungana na Waislamu wanapoendelea na mwezi mtukufu wa Ramadhan. Hata hivyo, serikali haifai ilegeze msimamo na sheria. Tunatarajia kwamba, wanapoadhimisha Ramadhan watazingatia kafyu na sheria nyinginezo wakati huu mgumu,” akasema Bw Kagwe.

Hata hivyo, Waziri huyo alieleza kamati hiyo kwamba, haiwezi kulegeza kafyu kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi wa kidini kukiuka sheria zilizowekwa na kuchangia kusambaa kwa virusi vya corona

Alisema imamu aliyekuwa akihubiri nyumba hadi nyumba mtaani Eastleigh alikuwa amekiuka agizo la wizara la kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona

Vilevile, alitaja mapadri wawili kutoka kaunti za Kitui na Siaya walisambaza virusi kaunti hizo.

Mapadri hao Nicholas Maanzo wa Kitui na Richard Oduor kutoka Siaya, hawakujitenga kwa siku 14 hata baada ya kusafiri kutoka Italia na baadaye wakapatikana na virusi vya corona.