Habari Mseto

Serikali yakataa kumfungulia bwanyenye akaunti zilizojaa mabilioni

September 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Richard Munguti

KAMPUNI ya bwanyenye Humphrey Kariuki anayeshtakiwa kwa kukwepa kulipa ushuru wa Sh41 bilioni imewasilisha ombi katika mahakama kuu agizo la kufunga akaunti za kampuni tisa iondolewe.

Jaji Jessie Lesiit alikataa kuamuru akaunti hizo zifunguliwe lakini akaamuru wakili Cecil Miller azikabidhi benki za Kenya Commercial (KCB) na National (NBK) nakala za kesi aliyowasilishwa chini ya sheria za dharura.

Akiomba mahakama ifutilie mbali maagizo ya kufungwa kwa akaunti hizo, Bw Miller , alisema wafanyakazi zaidi ya 3,000 katika makampuni husika wanakabiliwa na tisho la kufutwa kazi.

Bw Miller aliomba Jaji Lesiit aamuru kesi hiyo isikizwe hivi karibuni akidai, kesi dhidi ya Bw Kariuki na washukiwa wengine wanane imeorodheshwa kuanza kusikizwa Septemba 18, 2019.

Wakili Cecil Miller alipomwakilisha mteja wake mahakamani Septemba 10, 2019. Picha/ Richard Munguti

Pia alisema agizo la kufungwa kwa akaunti za ASL, Wow Beverages, Dalbit Petroleum Limited, Rhine Hart Limited, Section Investments Limited, Janus Continental Group Limited, Belgravia Construction Limited, Azalea Holdings Limited na, Kisima Management Company Limited lilitolewa kwa njia iliyo kinyume cha sheria na DPP.

Bw Miller alisema DPP alifululiza hadi mahakama ya Kiambu mnamo Agosti 16, 2019 baada ya kunyimwa agizo hilo na mahakama ya Milimani Nairobi.

Mahakama ilielezwa DPP alitumia mamlaka yake vibaya kuwashtaki washukiwa katika mahakama mbili tofauti kuhusu suala moja.

Wakili Miller (Kushoto) na wakili Benjamin Musyoki wakiwa nje ya korti baada ya kesi ya kufungwa kwa akaunti za kampuni tisa na DPP ya bwanyenye Humphrey Kariuki. Picha/ Richard Munguti

Kiongozi wa mashtaka Bi Catherine Mwaniki aliomba DPP na Inspekta Generali wapewe muda kujibu madai dhidi yao.

Kesi itasikizwa Septemba 17, 2019.