• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Serikali yakomesha ujenzi katika ardhi zinazozaniwa

Serikali yakomesha ujenzi katika ardhi zinazozaniwa

Na ALEX AMANI

SERIKALI imetangaza kwamba, haitaruhusu aina yoyote ya ujenzi katika ardhi zinazozozaniwa katika eneo bunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi.

Waziri Msaidizi wa Ardhi, Bw Gideon Mung’aro alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya wizara kupokea ruhusa kutoka kwa bunge la taifa kubainisha wamiliki halali wa ardhi hizo.

Bw Mung’aro alikuwa akizungumza katika wadi ya Sabaki wakati wa kumkabidhi rasmi mbunge wa eneo hilo, Bw Michael Kingi stakabadhi ambazo zimethibitisha kusitishwa kwa ujenzi katika ardhi zenye mizozo.

“Tumesitisha ujenzi wa aina yoyote katika ardhi zenye utata eneo hili, mpaka uchunguzi utakapofanyika na mwafaka kupatikana,’ alisema Bw Mung’aro.

Hata hivyo waziri huyo msaidizi alidokeza kwamba, licha ya kuwa huenda wizara hiyo ikashindwa kutatua matatizo ya ardhi kwa asilimia mia moja nchini, watazidi kujizatiti ili kuhakikisha wametatua asilimia kubwa ya matatizo hayo katika sehemu zote za nchi.

Kwa upande wake, mbunge wa Magarini aliitaka wizara ya ardhi kufutulia mbali hati miliki za ardhi za mabwenyenye wanaodaiwa kunyakua ardhi za wakazi eneo hilo.

Kulingana na Bw Kingi, suala la unyakuzi wa ardhi kwenye eneo bunge lake linaendelea kushuhudiwa katika maeneo tofauti huku wakazi wasio na uwezo wakizidi kudhulumiwa kila mara.

Wakati huo huo, mbunge huyo aliiomba serikali, kupitia Wizara ya Ardhi, na ile ya kaunti hiyo kusitisha shughuli zote za ujenzi katika ardhi ya Shirika la Ustawishaji Kilimo (ADC) inayokumbwa na utata hadi utata kuhusu umiliki wa ardhi hiyo utakapotatuliwa.

Ardhi hiyo ya ekari 900 imekumbwa na mzozo ikiwemo sakata ya unyakuzi unaoaminika kutendeka wakati wa utawala wa aliyekuwa rais, marehemu Daniel arap Moi.

Miongoni mwa wale waliotajwa kunufaika na unyakuzi huo ni wanasiasa mashuhuri na jamaa za Moi.’Tunaitaka serikali kutoa suluhu ya matitizo haya,’ alisema Bw Kingi.

Mbunge huyo pia aliwashutumu vikali baadhi ya viongozi katika kaunti hiyo akidai baadhi yao wamekuwa wakishirikiana na mabwenyenye kupora mali ya umma na kuwapokonya wakazi aridhi zao.

You can share this post!

Mgogoro wa Sudi ulivyofichua siri ya vita vya UhuRuto

MCAs wahimizwa kufuatilia matumizi ya fedha za kaunti