Habari Mseto

Serikali yaomba msaada wa sekta ya kibinasfi kukabili njaa

November 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imetoa wito kwa sekta ya kibinafsi kuisaidia kuwekeza katika kilimo kwa lengo la kuisaidia kukabiliana na ukosefu wa chakula kufikia 2022.

Akiongea wakati wa mkutano na washikadau katika sekta ya kibinafsi kuhusiana na utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya serikali(Big 4 Agenda), Waziri Msaidizi katika Wizara ya Kilimo Andrew Tuimur alisema uwekezaji katika kilimo na sekta ya umma hautoshi kukabiliana na ukosefu wa chakula nchini.

“Gharama kubwa ya kulima na mfumo dhaifu wa soko la mazao, ongezeko la watu, kupoteza zaidi baada ya kuvuna, mfumo usiostahili wa kilimo na mabadiliko ya anga ni changamoto kubwa zaidi katika uzalishaji wa chakula cha kutosha nchini,” alisema.

Ingawa Kenya imepanga kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh39.4 bilioni hadi Sh43.218 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2020-21, bado pesa hizo ziko chini sana, asilimia 2.4 pekee ya bajeti ya kitaifa, chini ya kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO) cha asilimia 10.

Kulingana na Bw Tuimur, nafasi iliyosalia katika kuhakikisha kuwa Kenya imefikia usalama wa chakula ni kwa sekta ya kibinafsi kuwekeza katika ukulima.