Habari Mseto

Serikali yaonya tiba ya corona isitumiwe ovyo

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

WANANCHI wameshauriwa dhidi ya kutumia dawa aina ya dexamethasone kutibu virusi vya corona bila idhini ya daktari.

Dawa hiyo ilibainika kupunguza makali ya virusi hivyo kwa watu walio hali mahututi kwa viwango mbalimbali, baada ya majaribio yaliyofanywa na wataalamu nchini Uingereza.

Mkurugenzi wa Matibabu nchini, Dkt Patrick Amoth jana alisema kutokana na kuwa dawa hiyo hupatikana kirahisi kwa bei nafuu, huenda baadhi ya wananchi wakaanza kuitumia kiholela wakishuku kuambukizwa virusi vya corona.

Serikali ilisema Kenya ingali inashauriana na taasisi za utafiti wa kimatibabu kubaini ikiwa dawa aina ya inafaa kwa matibabu ya ugonjwa wa Covid-19.

Hayo yalijiri huku idadi ya watu walioambukizwa virusi nchini ikifikia 4,044 baada ya visa 184 kuthibitishwa.

Idadi ya wale waliopona iliongezeka na kufikia 1,353 baada ya watu 27 zaidi kuruhusiwa kwenda nyumbani. Hata hivyo, watu wawili zaidi walifariki na kufikisha idadi kuwa 107.

Shirika la Afya Duniani (WHO) liliridhishwa na matokeo ya dawa hiyo, likisema yanaashiria huenda tiba ya virusi hivyo ikapatikana katika siku za hivi karibuni.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman alisema Kenya inafanya mazungumzo na WHO na taasisi zingine za kimatibabu, kubaini ufaafu wa dawa hiyo kwa matumizi ya wale walioambukizwa.

“Tunafuatilia kwa kina majaribio hayo. WHO imeeleza kuridhishwa na matokeo ya kwanza ya majaribio yake. Vivyo hivyo, tunashauriana na taasisi zetu za utafiti wa kimatibabu kubaini uhalisia wake kuihusu,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa Kenya itafuata taratibu zote za kimataifa kuhusu utafiti, kwani bado haijaidhinishwa rasmi kutumika.

Dawa hiyo husababisha madhara mwilini isipotumiwa ifaavyo. Baadhi ya madhara yake ni kuongeza uzani mwilini, ongezeko la shinikizo la damu, kisukari kati ya mengine.