Habari Mseto

Serikali yaonywa kutoa mikopo ya simu kutatupa Wakenya wengi CRB

June 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY WAWERU

Hatua ya serikali kutoa mikopo kupitia mtandao inahitaji mipango maalum. Aliyekuwa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo ameonya kuwa mikakati kabambe isipowekwa, huenda serikali ikapoteza fedha inazotoa.

Akitaja mpango huo kama “ubadhirifu na ufujaji wa mali ya umma”, mbunge huyo Jumatano alisema serikali inapaswa kuwa na maelezo kamilifu ya wanaokopa na jinsi fedha hizo zitakavyolipwa.

Midiwo alisema mikopo hiyo isitumiwe kuhangaisha vijana, ambapo wengi wa waliokopa kupitia apu za mashirika yanayotoa mikopo kupitia mitandao wamejipata kuorodheshwa katika CRB kwa kushindwa kulipa au kuchelewesha malipo.

“Benki zilizojukumika kutoa mikopo hiyo iwe na mpangilio maalum, ambapo mtu anapaswa kujaza maelezo kamilifu. Pia, serikali iwe na mikakati kabambe fedha inazotoa zitakavyoweza kulipwa,” alisema Bw Midiwo.

Mwezi uliopita, Mei, Benki Kuu ya Kenya-CBK kwa ushirikiano na benki zingine tano nchini ilizindua mpango wa utoaji mikopo kupitia simu ya mkono ili kupiga jeki wafanyabiashara wa wastani na wale wadogo wadogo, SMEs.

Kupitia apu ya Stawi, mteja anaweza kukopa kati ya Sh30, 000-250, 000. Mkopo unalipwa kati ya mwezi mmoja hadi 12, kwa riba ya asilimia 9 kwa mwaka.

Benki zilizoshirikiana na CBK kusimamia mikopo hiyo ni Cooperative, Diamond Trust Bank Kenya Limited (DTB), KCB na NIC.

Gavana wa CBK Dkt Patrick Njoroge Jumatano alifanya hamasisho la mikopo hiyo kaunti ya Kisumu.

Jakoyo Midiwo hata hivyo anasema licha ya serikali kuzindua mpango huo kuinua SMEs, inapaswa kuwa makini kwa kudhibiti usambaaji wa fedha ili taifa lisijipate katika hali tata ya uchumi dhaifu.

“Nchi kama India na China, serikali hudhibiti kiwango cha fedha inazoachilia katika uchumi ili uchumi usizorote,” alisema.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena mnamo Jumanne alitetea mpango huo akisema ni njia mojawapo ya mikakati ya serikali kuangazia ukosefu wa ajira nchini, hasa kwa vijana.

Aidha, Bi Kanze alisema vijana watatumia mikopo wanayopokea kuwekeza katika biashara.