SGR: Amri ya serikali kuathiri uchumi wa Mombasa
Na ANTHONY KITIMO
BIASHARA nyingi katika eneo la Pwani zitaathirika kufuatia amri ya serikali kwamba mizigo yote kutoka Mombasa hadi Nairobi isafirishwe kupitia Reli ya Kisasa (SGR).
Mnamo Ijumaa, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) na Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) zilisisitiza kuwa kuanzia Agosti 7 mizigo yote itasafirishwa kutoka bandarini hadi Nairobi kwa SGR wala sio kwa barabara ilivyo kawaida.
“Bidhaa zote zilizoagizwa kwa ajili ya kuwasilisha Nairobi na maeneo mengine ya bara itasafirishwa kwa SGR na kukaguliwa katika depo ya makonteina Nairobi na mizigo yote ya kwenda Mombasa na maeneo ya karibu ya karibu itakaguliwa katika bandari ya Mombasa,” notisi kwa umma ikasema.
Hatua hiyo itapelekea mamia ya wafanyakazi wa kampuni mbalimbali za kusafirisha mizigo (CFS) na maajenti wa kukagua bidhaa mjini Mombasa kukosa kazi. Hii ni kwa sababu takriban asilimia 85 ya bidhaa zilizoagizwa kutoka ng’ambo zitakaguliwa jijini Nairobi.
Wadau mbalimbali katika sekta ya uchukuzi wa mizigo wamepinga hatua hiyo ya serikali, wakisema inakwenda kinyume na mkataba wa Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) unahitaji kwamba mizigo isafirishwe bila vikwazo, na kwa gharama nafuu.
Mkataba
Kenya ilitia sahihi mkataba huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Kimataifa ya Wasafirishaji na Wenye Mabohari (KIFWA) Roy Mwanthi jana alisema chama hicho kitatoa malalamishi yake rasmi kwa serikali kuhusu athari za amri hiyo kwa biashahara zao.
“Hatua hii itaua kampuni zote za uchukuzi wa bidhaa kutoka bandarini (CFS) hali ambayo itaathiri pakubwa uchumi wa Mombasa, kwani maelfu ya wakazi watapoteza ajira,” akasema Bw Mwanthi.
Zaidi ya kampuni 20 za CFSs ambazo zimewekeza takriban Sh12.5 bilioni katika eneo hili na zinamiliki zaidi ya malori 800 Mombasa huenda zikakosa biashara ikiwa amri hii itatekelezwa, hivyo maelfu watasalia bila kazi.
Vyumba vya malazi na mikahawa ambayo wateja wao wengi na wahudumu wa biashara ya uchukuzi wa mizigo pia watapoteza pakubwa, sio tu eneo la pwani bali miji mingine iliyoko kando mwa barabara ambayo hutumiwa na matrela ya mizigo.