• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
SGR: Hisia mseto zaibuka Magharibi Rais akikosa mkopo

SGR: Hisia mseto zaibuka Magharibi Rais akikosa mkopo

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI na wafanyabiashara wa maeneo ya Magharibi mwa Kenya wametofautiana vikali kuhusu hatua ya Rais Uhuru Kenyatta, kukosa kupata fedha za mkopo kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) , kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Wengine wanasema mkopo huo ungekuwa mzigo kwa walipa ushuru huku baadhi wakidai ungesaidia kuinua hali ya uchumi wa wakazi wa Magharibi mwa Kenya.

Rais Kenyatta aliongoza ujumbe wa Kenya, uliojumuisha pia kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuelekea nchini China wiki iliyopita, lakini wakashindwa kupata mkopo kwa ajili ya ujenzi wa reli ya SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Serikali sasa imeelekeza juhudi zake katika kukamilisha ujenzi wa SGR kutoka Nairobi hadi Naivasha na kisha kuiunganisha na reli za zamani hadi Magharibi mwa Kenya.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara tawi la Kisumu, Bw Israel Agina, alisema kuwa reli hiyo ya SGR ingesaidia kuboresha hali ya uchumi wa wakazi wa Magharibi mwa Kenya.

“Wakoloni walibaini umuhimu wa jiji la Kisumu na ndiyo maana walijenga reli ya kutoka Mombasa hadi Kisumu. Eneo la Magharibi bado halijastawi kimiundomsingi,” akasema Bw Agina.

“Hata hivyo, kukarabatiwa kwa reli ya zamani kutoka Naivasha hadi Kisumu bado kutasaidia jiji la Kisumu kustawi kiuchumi,” akaongezea.

Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o alisema kuwa mradi wa SGR ungesaidia kuwapa nafasi za kazi wakazi wa Kisumu na maeneo mengineyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Magharibi mwa Kenya, Bw Robinson Anyal, naye alisema kuwa reli hiyo ingewezesha idadi kubwa ya watalii kuzuru ukanda huo.

“Reli hiyo ya SGR ingeunganisha maeneo ambayo ni vivutio vya watalii kama vile Mombasa, Naivasha, Maasai Mara na vivutio vya Magharibi mwa Kenya kama vile Kisiwa cha Ndere Ndere, Ziwa Victoria, Kit Mikayi ana msitu wa Kakamega kati ya vivutio vinginevyo,” akasema Bw Anyal.

Alieleza kuwa muafaka wa ushirikiano baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga umesaidia kuinua sekta ya utalii humu nchini.

“Tangu viongozi hao walipoafikiana kufanya kazi pamoja, kumekuwa na utulivu nchini hivyo kuvutia watalii wengi kuzuru Kenya,” akasema.

Mbunge wa Kisumu Magharibi, Bw Olago Aluoch amesema kuwa reli ya zamani itasaidia kuinua uchumi wa ukanda huo endapo itakarabatiwa.

Lakini aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Khalwale na waziri wa zamani wa Michezo, Bw Rashid Echesa, walishutumu Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa kutumia ushirikiano wao kuwatwika mzigo Wakenya.

Dkt Khalwale alidai kwamba Rais Kenyatta na Bw Odinga wanatumia ushirikiano wao kupeleka miradi ya katika ngome zao za kisiasa na kupuuza maeneo mengine.

Kwa wakati huu huduma za reli hiyo ya kisasa zinapatikana kwa wanaosafiri kati ya Nairobi hadi Mombasa.

Ripoti za JUSTUS OCHIENG, CAROLINE MUNDU na SHABAN MAKOKHA

You can share this post!

Sonko adai anachafuliwa jina kwa kukataa kutoa hongo

Maambukizi ya HIV kutoka kwa mama hadi mtoto yaongezeka

adminleo