SGR: Mizigo imeleta faida, abiria wamepungua – Ripoti
Na ALLAN OLINGO
BIASHARA ya kubeba mizigo kutumia reli mpya (SGR) ililetea nchi mapato ya Sh7.54 bilioni ikibeba tani 3.25 za mizigo kwa kipindi cha miezi tisa kufikia Septemba 2019, ripoti imeeleza.
Hata hivyo, ripoti hiyo imeonyesha kuwa upande wa uchukuzi wa mizigo uliimarika huku idadi ya watu wanaosafiri kupitia treni ikipungua kwa watu 200, 000.
“Idadi ya abiria wanaotumia SGR ilipungua kutoka 1.38 milioni kwa kipindi kama hicho mwaka wa 2018 hadi 1.18 milioni mwaka jana,” ikasema ripoti.
Hii inaashiria kuwa sheria kali zilizowekwa katika saa za kuabiri treni na ushindani kutoka kwa kampuni za mabasi na ndege zinazolipisha bei nafuu zimewafanya abiria wengi kuacha kutumia SGR.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) kama ilivyotolewa na Shirika la Reli, mapato ya Sh4.09 bilioni ya biashara ya kubeba mizigo na SGR kwa miezi hiyo tisa ya mwaka jana, ilikuwa mara mbili ya mwaka wa 2018.
Mapato hayo yalikuwa yaongezeke Aprili mwaka jana baada ya Shirika la Reli Nchini kusitisha bei ya kuvutia wateja na kusema kuwa bei ambazo zilipitishwa kwa makubaliano ya wizara ya uchukuzi na Halmashauri ya Bandari Nchini(KPA)ziendelee.
Wafanyabiashara walianza kulipa Sh51, 275 kwa kasha la futi 20 na Sh70,000 kwa kasha la futi 40 ambayo ni mara mbili ya bei ya mvuto ya Sh25,000 hadi Sh35,000.
Hii ina maana kuwa nchi ilipata zaidi ya Sh10 bilioni mwaka jana kutoka kwa biashara hiyo ya kusafirisha mizigo, ambayo bado iko chini sana kulingana na gharama ya mwaka mzima ya Sh18 bilioni ya kufanya ukarabati.
“Shirika la reli na kampuni ya ujenzi ya China Communications Construction Company zilipata Sh1.15 bilioni kutoka kwa tani 430,450 ya mizigo iliyosafirishwa mwezi wa Agosti. Mwezi wa Februari, mashirika hayo yalipata mapato ya chini kabisa ya Sh435.18 milioni,” ikasema ripoti.
Hata hivyo, kiwango kuongezeka kwa mapato hayo bado kiko chini ya kiwango ambacho shirika linalenga kwa kuwa bado idadi ya treni zinazotoka Mombasa kuelekea Nairobi ni zilezile.
Hii ni kwa sababu nafasi ya kuweka mizigo katika eneo la Embakasi ni ndogo, bei ya juu ya kusafirisha mizigo na matumizi kidogo ya stesheni ya Nairobi inashughulikia mizigo ambayo haijawekwa upande wa makasha.
Ongezeko la mapato haya kutokana na biashara ya SGR kusafirisha mizigo limetokea wakati ambapo mashirika ya kibinafsi na wafanyibiashara ikiwemo wanaoshughulikia mizigo hiyo, wamekuwa wakiandamana kuanzia Agosti mwaka jana, baada ya serikali kuamuru kuwa mizigo yote isafirishwe kwa reli.
Mwezi Januari, aliyekuwa Katiba wa Uchukuzi, Bi Esther Koimett alikanusha madai ya kuhusika kwa serikali katika mpango wa wafanyibiashara kusafirisha mizigo kwa reli. Alidai kuwa kuna uwezekano kwamba hali hiyo imechangiwa na gharama ya chini ya kusafirisha.
Alisema waagizaji mizigo kutoka ng’ambo wako huru kuamua kama watasafirisha mizigo yao kwa malori (barabara) au kutumia SGR.
“Kama mtakumbuka, agizo la kuwataka wasafirishe mizigo kutumia SGR lilisimamishwa. Tunafurahi kuwa wafanyibiashara wenyewe wameona afueni iliyopo kwa kusafirisha kutumia SGR ikilinganishwa na njia nyingine za uchukuzi,” akasema.