Sh150m zawekezwa kuzima wadukuzi mitandaoni
Na BERNARDINE MUTANU
Kutokana na ongezeko la uvamizi wa mitaliga (virusi), udukuzi, wizi wa hela na data ya siri mitandaoni humu nchini na kwingineko, wataalamu sasa wameamua kukabiliana nao kikamilifu.
Kituo cha kufunza wataalamu wa kukabiliana na visa hivyo kinaendelea kujengwa nchini, mjini Thika.
Kituo hicho kitakachogharimu kampuni ya Yelbridges Sh150 milioni kinalenga kuwafunza wataalam wa Habari na Mawasiliano (IT) jinsi ya kukabiliana na vitisho mitandaoni nchini.
Kituo hicho kitakuwa cha kisasa na kitawezesha watakaopewa mafunzo kuwa na uwezo wa kujua jinsi udukuzi wa kimitandao hutekelezwa na jinsi ya kujilinda, kukabiliana na tukio na mambo mengine.
“Kulingana na ripoti kuhusiana na usalama wa mitandaoni, asilimia 96 ya visa vya uvamizi mitandaoni huwa haviripotiwi au huwa havitatuliwi. Hayo ni baadhi ya mambo yatakayolengwa na kituo hicho,” alisema afisa wa operesheni wa Yelbridges Steve Mambo.
Aliongeza kuwa Africa, kuna wataalam chini ya 10,000 wa uvamizi wa kimtandao dhidi ya watu zaidi ya 1.3 bilioni barani.
“Eneo la Afrika Mashariki halina wataalam wengi kuhusiana na suala hilo na jinsi ya kujikinga,” alisema, na kuongeza kuwa hilo lilikuwa kiini cha kuanzisha kituo hicho.
Utafiti wa hivi majuzi unaonyesha kuwa asilimia 90 ya taasisi Kenya huwa zinafanya operesheni zake chini ya kiwango kinachohitajika cha usalama wa kimtandao.
Kwa sasa, kiwango cha uhalifu wa kimtandao kimepanda kutoka Sh200 bilioni 2016 hadi Sh350 bilioni mwaka wa 2017.