Habari Mseto

Sh500 milioni kwa atakayefichua aliko Jehad Serwan Mostafa

December 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WAMBUI

Idara ya upelelezi ya Amerika (FBI), imetoa zawadi ya Sh500 milioni kwa yeyote atakayetoa habari zitakazofanikisha kukamatwa kwa Jehad Serwan Mostafa, raia wa nchi hiyo mwenye umri wa miaka 37 ambaye inaaminika amekuwa akifadhili shughuli za Al Shabaab, Afrika Mashariki.

Mostafa, anayezungumza Kiarabu, Kisomali na Kiswahili pia anajulikana kama Ahmed Emir Anwar, Ahmed Gurey, Anwar al-Amriki na Abu Adbullah al-Muhajir.

Ikimtaja kama mtu hatari, idara hiyo ilisema inaamini mshukiwa huyo ndiye raia wa cheo cha juu wa Amerika ambaye amekuwa akifadhili shughuli za kijeshi za kundi la Al Shabaab tangu 2006.

Majukumu yake katika Al Shabaab ni pamoja na kutoa mafunzo katika kambi za Al Shabaab, kueneza propaganda za kundi hilo, kuongoza mashambulizi ya vilipuzi na kuwa wakala kati ya kundi hilo na mashirika mengine ya kigaidi.

FBI inaamini kuwa, Moustafa ametembelea au anapanga kutembelea Somalia, Yemen, Kenya na mataifa mengine ya Afrika ili kuendeleza vitendo vya kundi hilo la kigaidi.

Anafunga ndevu kubwa na kufaa miwani na anatumia mkono wa kushoto na ana kovu katika mkono wake wa kulia.

“Ikiwa una habari zozote kuhusu mtu huyu, tafadhali wasiliana na ubalozi wa Amerika ulio karibu,” linasema tangazo katika tovuti ya FBI.

Tangazo hilo linasema alilelewa San Diego, California, ambako pia alisomea chuo kikuu.Inaaminika alihama alikozaliwa 2005.