• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
SHAIRI: Ukapera siachi, muhibu sipati

SHAIRI: Ukapera siachi, muhibu sipati

Na FELIX GATUMO

NAAMUA kwa hiari, kutoasi ukapera,

Mahaba kwangu kwaheri, sitaki tena hasara,

Akili yameathiri, yamenifyonza humra,

Mola sinipe mapenzi, kwani wa kupenda sina.

Kusema sitakawia, ni mengi yalonikumba,

Magumu nimepitia, kiini chake uchumba,

Taishi kuhadithia,’lonitenda mahabuba,

Mola sinipe mapenzi, kwani wa kupenda sina.

Najuta kugharamika, hili niweze kupendwa,

Baadaye kuachika, ‘lipojuwa ninapondwa,

Mawazoni natafrika, nalia mimi kuachwa,

Mola sinipe mapenzi, kwani wa kupenda sina.

Huyu habibi wangu, sikujuwa hanipendi,

Nilimpa penzi langu, Maulana ni shahidi,

Meatuwa moyo wangu, mwengine tena sipendi,

Mola sinipe mapenzi, kwani wa kupenda sina.

Kwangu ameshaondoka, mpweke ameniacha,

Mabwanyenye memteka, penzi kwao limechacha,

Adawa wananicheka, ninalia kutwa kucha,

Mola sinipe mapenzi, kwani wa kupenda sina.

Hisia wenzangu sina, yamenitoka mapenzi,

Nimeasi kupendana, kurudi nyuma siwezi,

Ubinadamu hawana, baadhi yao wapenzi,

Mola sinipe mapenzi, kwani wa kupenda sina.

Felix Murangiri Gatumo

Malenga Mtamu

Chuo Kikuu Cha Maseno.

You can share this post!

AFCON2019: Limbukeni wawili kuramba urojo wa soka ya bara

KURUNZI YA PWANI: Msikiti wa Riyadha kufundisha dini ya...

adminleo