SHAMBULIO: Wanao Khalwale na Mudavadi wanusuriwa
Na PETER MBURU
FURAHA ilitanda nyusoni mwa viongozi Boni Khalwale, Musalia Mudavadi na Beatrice Adagala (Mwakilishi mwanamke wa kaunti ya Vihiga), baada ya wanao ambao walikuwa mateka kufuatia vamizi katika hoteliya Dusit eneo la Riverside Jumanne kuokolewa.
Dkt Khalwale, seneta wa zamani wa Kakamega alikuwa amepiga kambi eneo hilo tangu Jumanne jioni kwa Imani kuwa bintiye, ambaye ni mfanyakazi wa kampuni moja eneo hilo, angetoka akiwa mzima.
Na kama majibu ya maombi yake, mwendo was aa tisa na dakika 38 alfajiri ya Jumatano, bintiye aliokolewa kutoka jingo hilo, matokeo yake yakiwa machozi ya furaha usoni mwa babake.
Dkt Khalwale alieleza wanahabari kuwa bintiye alimpigia simu mara tu vamizi hilo lilipoanza, dakika chache baada ya saa tisa jioni, Jumanne.
“Alinipigia mara tu milio ya bunduki ilipoanza. Nilikuwa uwanja wa ndege wa JKIA na nilirudi mara moja hadi huko. Alikuwa akiniambia kila mara kuwa milio ya risasi ilikuwa ikiwakaribia, jambo ambalo lilinishtua. Anafanya kazi hapa lakini siwezi kusema na kampuni gani kwa sababu za usalama,” akasema Dkt Khalwal;e.
Ni hapo ambapo aidha alidokeza bila maelezo mengi kuwa vijana wa kiume wa Musalia Mudavadi, kiongozi wa ANC na Bi Adagala vilevile walikuwa ndani wakati wa vamizi, lakini wakaokolewa.
”Mvulana wa Mudavadi alikuwa hapa lakini akaokolewa na polisi saa kumi na moja jioni naye wa Adagala akaokolewa saa moja baadaye,” akasema kiongozi huyo.