SHANGAZI: Hasemi nami tena tangu nikatae kumburudisha kitandani
Naomba ushauri wako Shangazi. Nilipiga nambari fulani ya simu kimakosa na ikapokewa na kijana. Nilipomwelezea kuwa niliipiga kimakosa alinitania kuwa nilipigia mtu aliyefaa. Tuliendelea kuwasiliana na hatimaye tukawa wapenzi kupitia kwa simu. Wiki iliyopita tulikutana kwa mara ya kwanza na akaniomba asali nikakataa. Tangu siku hiyo amekasirika hataki kuongea nami. Nifanyeje?
Kupitia SMS
Kijana huyo ni tapeli wa kimapenzi, muepuke mara moja. Sababu ni kuwa alikurukia ghafla siku ya kwanza ulipopiga simu yake kimakosa na papo hapo akakutupia chambo eti anakupenda ilhali hakujui wala hakutambui. Siku ya kwanza kukuona anataka asali! Je, unafikiri kesho akipigiwa na mwingine kama wewe atamuacha? Naona wewe ni mgeni kwa wanaume, nenda taratibu.
Nasaka mpenzi wa kiume
Kwako Shangazi. Samahani kama utaona vibaya kwa ombi langu kwako. Mimi ni mwanamume na naomba kama unaweza kunitambulisha kwa mwanaume ambaye angetaka kuwa na mwenziwe maishani. Kupitia SMS
La, hasha! Mimi kamwe siungi mkono mahusiano kama hayo wala sitawahi. Msimamo wangu ni kuwa uhusiano halali ni kati ya wanaume na wanawake. Pili, kazi yangu katika ukumbi huu ni kutoa ushauri wala si kutafutia watu washikaji.
Aishi mbali na ni bahili
Shikamoo Shangazi. Nina husiano na kijana fulani lakini nahisi uhusiano wetu hautaenda mbali kwani anaishi mbali na imekuwa shida kupata usaidizi wake ninapouhitaji. Nishauri. Kupitia SMS
Hiyo ni mojawapo ya changamoto za uhusiano kati ya mtu anayeishi mbali na mwenzake. Kuna baadhi ya watu wanaofaulu kudumisha uhusiano kama huo na hatimaye kufunga ndoa ilhali wengine hulemewa na kutafuta maisha kwingine. Kauli yako inaonyesha umeanza kulemewa na una haki ya kujiondoa katika uhusiano huo iwapo unahisi hauna manufaa kwako.
Anahepa ndoano yangu
Shangazi pokea salamu zangu za dhati. Kuna mwanamke ambaye ninampenda sana na anajua hivyo kwani nimemwambia mara kadhaa. Badala yake ananionyesha dharau. Naomba ushauri wako. Kupitia SMS
Ninaamini kuwa wewe ni mtu mzima na kuna mambo unayofaa kuona ama kusikia na kuelewa maana yake. Hali kwamba umemdokezea hisia zako mwanamke huyo na badala ya kukubali ombi lako anakudharau ni ishara kamili kuwa hana haja nawe. Je, unasubiri hadi akwambie hivyo ndivyo uelewe? Shauri yako!
Haonyeshi kwa vitendo
Kwako Shangazi. Kuna mwanamume ambaye nimempenda kwa moyo wangu wote, huu sasa ni mwaka wa pili. Yeye pia ananiambia ananipenda lakini hanionyeshi penzi lake kwa vitendo. Nipe ushauri. Kupitia SMS
Hujaelezea unatarajia vitendo gani kutoka kwa mwanaume huyo ili kuthibitisha penzi lake kwako. Kama unajua unachotaka na hujamwambia, hakuna jinsi ambavyo atajua kwani yeye si malaika. Ni muhimu umwelezee badala ya kulalamika kimya kimya.
Simu yake aniita kijana
Habari yako Shangazi. Nimemsaidia msichana mpenzi wangu kwa hali na mali hadi amefuzu mafunzo ya ualimu. Ajabu ni kuwa huwa hapendi nimtumie SMS lakini nikikagua simu yake napata SMS za wanaume wengine wawili. Katika simu yake ananitambua tu kama ‘kijana’ ilhali hao wengine anawatambua kama ‘sweery’ na ‘beiby’. Mimi naona ananichezea. Waonaje wewe? Kupitia SMS
Mwenye macho haambiwi tazama. Huo hasa ndio ukweli wa mambo na uchunguzi wako umethibitisha. Majina anayowatambua kwayo wanaume hao wawili yanaonyesha kuwa amewapa nafasi maalumu moyoni mwake kuliko wewe anayekutambua kama ‘kijana’. Sasa ni wakati wa kumuondokea aendelee na sarakasi zake.
Tangu nifutwe sichovyi
Nina umri wa miaka 29. Nimeoa na nimejaliwa watoto wawili. Tatizo ni kwamba, mke wangu ananinyima mapenzi kisa nimesimamishwa kazi. Nimejaribu kumshauri na wiki mbili sasa sijafanya lolote kwake. Hassan. Mombasa. Kupitia SMS
Mbali na mapenzi na mengine katika ndoa, mwanamke pia hutarajia uhakika na usalama wa maisha yake kupitia kwa mumewe. Hivyo inawezekana baada ya kusimamishwa kazi mkeo ameingiwa na baridi yabisi aidha ya hofu ya kupoteza malazi ama yale aliyokuwa anapata wakati ukiwa kazini. Jaribu kuzungumza naye umtoe hofu na umhakikishie upendo wako kwake. Pia umuulize kama anataka kukueleza lolote kuhusiana na hali ilivyo sasa.