Sherehe za Leba Dei zakosa ladha Wakenya wakiendelea na shughuli zao
WAKENYA katika kaunti nyingi walisusia maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi iliyoadhimishwa jana, wakisema hawakuwa na chochote cha kusherehekea.
Hakukuwa na hafla za umma katika kaunti nyingi huku serikali za kaunti zikishindwa kushawishi wakazi kushiriki siku hiyo inayoadhimishwa kutambua mchango wa wafanyakazi.
Katika kaunti za Nyeri na Kirinyaga, wakazi waliendelea na shughuli zao za kila siku bila kujali kabisa siku hiyo.
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema hakukuwa na chochote cha kufurahia kwa sababu Wakenya wanaendelea kuumia kutokana na uchumi mgumu ndani ya utawala huu.
“Hata siku ya wafanyakazi inapoadhimishwa kwa miaka ya 60, simulizi ya mfanyakazi inasalia ile ile: uchungu, mahangaiko na mateso. Tunajua hakuna Mkenya ambaye anafurahi na kuwatakia Leba Dei njema ni kuwaongezea tu ushuru,” akasema Bw Gachagua.