Habari Mseto

Sheria za vyama vya ushirika zibadilishwe, wasema wafugaji

September 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

STANLEY KIMUGE na W. KIPSANG

WAFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa sasa wanataka sheria zinazoongoza utendakazi wa vyama vya ushirika nchini ziangaziwe upya ili kuvisaidia visiporomoke kutokana na usimamazi mbaya.

Kwa mujibu wa wakulima, sheria mpya zinafaa zitungwe ili kuboresha sekta ya ufugaji na mauzo ya maziwa nchini. Chama cha Wakulima Nchini (KDFF) nacho kilisema sheria hizo mpya zitahakikisha Wakenya wanauziwa maziwa bora kwa kuwa ng’ombe watalishwa vyakula vizuri na mbinu za kisasa za uzazi kutumika kuimarisha ufugaji.

“Sheria zetu za vyama vya ushirika zina ulegevu mwingi na baadhi hata vinasimamiwa kupitia mfumo wa demokrasia ndiyo maana vinaanguka. Vyama vya ushirika ambavyo bado ni imara navyo vimewawekea malengo wafugaji kuwasilisha lita 50 za maziwa huku pia wakinunua hisa na kuchangia usimamizi vyema wa vyama hivyo,” akasema mwenyekiti wa bodi ya KDFF Henry Otyula.

Mwezi uliopita bodi ya maziwa nchini (KDB) ilipendekeza mpango wa kuwafungia nje mabroka na wasafirishaji wa maziwa ambao huwalaghai wakulima wafugaji fedha zao.

“Serikali imewekeza fedha nyingi za kununua mashine au vifaa vya kuhifadhi maziwa. Hii ndiyo maana tunataka vyama vya ushirika visimamiwe vizuri na mwishowe vijisimamie. Baadhi ya sheria zimesaidia katika ufanisi wa vyama vya ushirika katika baadhi ya maeneo na kukosa katika maeneo mengine kutokana na siasa,” akaongeza Bw Otyula.

Mkurugenzi msimamizi wa KDB Margaret Kibogy aliunga wito huo wa sheria mpya kutumika, akisema itawasaidia wakulima kutolipa gharama za usafiri.

“Sekta ya ufugaji wa ng’ombe za maziwa na mauzo ya maziwa hayo yataimarika zaidi. Tunafaa kuanza kukumbatia mtindo wa kisasa wa kusimamia vyama vyetu vya ushirika na pia ufugaji,” akasema Bi Kibogy.

Kama kawaida wasafirishaji huchukua maziwa kutoka kwa wakulima kisha kuyauza kwa maduka na kampuni na baadaye wakulima hulipwa baada ya Sh3 kutozwa kwa kila lita kama gharama ya usafiri.

Wakulima pia wameirai serikali kuwapa lishe asili ya mifugo ili kuwaondolea gharama kubwa ya ufugaji.

“Huwa tunapata lishe asili kama pamba, soya na vyakula vingine vya mifugo kutoka mataifa mengine hali ambayo inapandisha gharama ya ufugaji. Kwa kila lita ya maziwa inayokamuliwa, mkulima hutumia Sh25 na hii ina maana kwamba mkulima huhitaji alipwe Sh34 orSh35 ndipo apate faida,” akasema mfugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka Kaunti ya Uasin Gishu David Kipchumba.

Tangu mwezi Januari, wizara ya kilimo imetumia Sh2.2 bilioni kununua mashine 350 za kuhifadhi maziwa huku kila mashine ikiwa na uwezo wa kuhifadhi lita 3,000.