Shirika latuzwa Sh15m kwa kuvumbua teknolojia ya kilimo
Na VALENTINE OBARA
WAKATI ambapo mabilioni ya watu ulimwenguni hutumia mitandao ya kijamii kwa mawasiliano ya kawaida na burudani, kuna wataalamu nchini walioona nafasi ya kutumia mitandao hiyo kusaidia wakulima.
Uvumbuzi wa shirika la Farm.ink linalopatikana Nairobi, ulipelekea shirika hilo kutuzwa dola 150,000 (Sh15 milioni) wiki iliyopita kwenye shindano la kutafuta uvumbuzi bora zaidi wa kupambana na viwavijeshi.
Shindano hilo lililoandaliwa na Shirika la Amerika la kutoa misaada kimataifa (USAID), lilikuwa limevutia wavumbuzi wa teknolojia za kisasa kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni kote.
Farm.ink imekuwa ikitumia mitandao ya kijamii, hasa programu ya ‘Messenger’ inayomilikiwa na Facebook, kutoa huduma zinazowezesha wakulima kukabiliana na viwavijeshi ambao walisababisha hasara kubwa kwa wakulima wa mahindi nchini mwaka uliopita.
Shirika hilo huwa limekusanya wakulima na wataalamu kwenye kikundi kinachotambulika kama ‘Africa Farmers Club’ kwenye programu ya Messenger, ambapo wakulima wadogo hupata fursa ya kujifunza kuhusu mbinu mwafaka za kujiepushia hasara.
Maelezo kuhusu mfumo huu ni kwamba wanapokuwa katika kikundi hicho cha Messenger kilicho na wakulima zaidi ya 150,000 kutoka mataifa mbalimbali Afrika, wakulima hupokea mafunzo maalumu inayowaongoza kuhusu jinsi ya kutambua hatari ya uvamizi wa viwavijeshi, na kupewa mapendekezo kuhusu mbinu za kuangamiza wadudu hao endapo tayari wamevamia mashambani.
Mbinu hii isiyo na gharama huhitaji mkulima awe na simu pamoja na intaneti, na hana haja kusafiri maeneo ya mbali kutafuta ushauri wa kitaalamu.
Zaidi ya hayo, kutokana na kuwa wakulima wengi hueleza matatizo tofauti, ushauri wa kitaalamu huwa umezingatia matatizo yote yaliyopo na hivyo basi ushauri unaotolewa huwa wa kikamilifu.
Kwa kutumia teknolojia ya kisasa, shirika hilo huwa limeandaa majibu sahihi kwa kila swali la mkulima kupitia uchanganuzi wa maswali sawa na hayo ambayo yalikuwa yameulizwa awali na hivyo basi mkulima hatakikani kusubiri muda mrefu kupata majibu ya changamoto zinazomkumba shambani.
Kwa mujibu wa shirika hilo, lengo kuu la Farm.ink ni kuhakikisha wakulima wadogo wanapata ushauri sahihi wanaohitaji kuhusu kilimo bora kwa haraka, na bila kutumia gharama kubwa.