Habari Mseto

Shule zote za umma kuvalia sare za rangi moja

July 9th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

WYCLIFF KIPSANG na CHARLES WASONGA

SERIKALI imetangaza nia ya kubadilishwa kwa sera ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wa shule zote za umma watakuwa wakivalia aina moja ya unifomu.

Katibu wa Wizara ya Elimu, Belio Kipsang Jumapili alisema serikali imeanzisha mazunguzo na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa shule zote zinatumia aina na rangi moja ya sare.

“Kampuni za kutengeneza nguo nchini, ikiwemo Rivatex iliyoko Eldoret zitatwika jukumu la kutengeneza sare mpya wakati ambapo tutaanza kutekeleza sera hii mpya,” Dkt Kipsang akasema akiwa mjini Eldoret.

Alizitaka kampuni za nguo kujiandaa ili zipewe kandarasi ya kutengeneza unifomu ambazo zitatosheleza wanafunzi katika shule zote za umma.

Shule za msingi na za upili nchini zimekuwa na sera na miongozo tofauti kuhusu sare za wanafunzi, ambapo kila shule imekuwa na unifomu tufauti. Kwa hivyo, kufuatia tangazo la Dkt Kipsang’ shule hizo zitalazimika kubadili sera hizo kwa kukumbatia aina moja ya sare.

Sera hii inayopendekezwa na Wizara ya Elimu inatumika nchini Ghana ambapo wanafunzi wa shule zote za umma huvalia sare zinazofanana. Tofauti katika sare hizo huwa ni nembo ya shule ambayo huchapishwa kwa kutumia rangi tofauti.

Mpango wa kuanzishwa kwa sera mpya ya unifomu unajiri miezi michache baada ya aliyekuwa Waziri wa Elimu Fred Matiang’i kutoa amri kwamba mabasi yote ya shule yapakwe rangi ya manjano.

Dkt Kipsang, ambaye alikuwa akiongea alipozuru kiwanda cha kutengeneza ngua cha Rivatex kinachomilikiwa na Chuo Kikuu cha Moi, alipongeza chuo hicho kwa kuchangia juhudi za kufufua kumpuni hiyo, hatua ambayo alisema imeimarisha ongezeko la nafasi za kazi.

Dkt Kipsang alikariri kwamba serikali imejitolea kuendelea kuwekeza rasilimali nyingi katika taasisi za mafunzo nchini.

“Taasisi kama hizi zinachangia pakubwa katika kuzalisha nguvu ambayo taifa hili linahitaji kuchochea ukuaji wa kiuchumi nchini. Taasisi za kielimu zinachangia pakubwa kuisaidia serikali katika azma yake ya kutimiza Ajenda zake Nne Kuu zilizotangazwa na Rais,” akasema Dkt Kipsang.