Habari Mseto

Shule 332 za udereva kufungwa kote nchini

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

VITUO 332 vya kutoa mafunzo ya udereva nchini vitafungwa kwa kutotimiza kanuni zinazohitajika, Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ameagiza.

Kuna jumla ya vituo 600 vya kutoa mafunzo ya udereva nchini.

Akihutubu jana kwenye Kongamano Maalum la Usafiri lililoandaliwa na mamlaka ya NTSA jijini Nairobi, Dkt Matiang’i alilalamika kuwa vituo vingi vimekuwa vikiendesha utoaji mafunzo hata bila magari ya kufunzia.

“Ni masikitiko kuwa baadhi ya vituo havina hata magari ya mazoezi. Vingine vina magari makuukuu, huku yule anayetoa mafunzo akiwa mtu mzee ambaye hata hana ufahamu wowote kuhusu kanuni za kisasa za barabarani. Hatuwezi kuendelea kuhatarisha maisha ya Wakenya kwa njia hiyo,” akasema.

Mnamo Aprili, waziri aliviagiza vituo hivyo kusajiliwa upya na NTSA ili kupewa leseni mpya za kutoa mafunzo. Vituo hivyo pia vilipewa hadi Julai 1, kutimiza kanuni zote zinazohitajika na serikali.

Kufuatia ukaguzi ambao uliendeshwa na NTSA, waziri alisema waligundua baadhi ya mafunzo yanayotolewa na baadhi ya vituo hivyo hayalingani na mtaala wa mafunzo ya udereva ulioidhinishwa.

“Hilo ndilo limekuwa kiini cha ajali nyingi ambazo tumekuwa tukishuhudia, kwani madereva wengi wanapewa leseni hata bila kufanya majaribio ya kuendesha gari hata kidogo. Huu ni mtindo ambao lazima ukome,” akasema Dkt Matiang’i.

Mkurugenzi Mkuu wa NTSA, Bw Francis Meja alisema kuwa operesheni hiyo ya kufunga shule hizo itaanza mara moja.

Kulingana na takwimu, Wakenya 3,000 hufariki kila mwaka kutokana na ajali za barabarani.